Jan 18, 2019 16:12 UTC
  • John Pombe Magufuli
    John Pombe Magufuli

Rais John Pombe Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema kuwa, kama kuna changamoto ambazo bado hazijafanyiwa kazi katika uongozi wake, basi hana uhakika iwapo kiongozi atakayekuja baada yake atakuwa na uwezo wa kuzitatua.

Magufuli ameyasema hayo leo katika hafla ya makabidhiano ya mfumo wa kusimamia uwazi katika mawasiliano ya simu (TTMS) wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). Rais wa Tanzania amesema kuwa, katika safari ya kutatua changamoto za nchi hiyo anakumbana na mambo mengi magumu na kwamba ndio sababu amekuwa akihitaji nguvu za Mungu kutekeleza majukumu yake. “Viongozi wa dini endeleeni kuliweka taifa hili kwenye mikono ya Mungu. Hii ni vita kama ilivyo nyingine na vita ya uchumi inahitaji maombi sana, bila maombi kazi hii haiwezi kufanyika”, Amesema John Magufuli.

Wakati huo huo Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amemueleza Rais Magufuli kuwa bunge lake si dhaifu kama alivyosema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu na Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad.

Mvutano kati ya CAG, Profesa Mussa Assad, Spika wa Bunge Job Ndugai na Zitto Zuberi Kabwe

Akizungumza katika hafla hiyo Ndugai amesema kuwa, utekelezaji wa mradi huo ulitegemea sana maoni ya wabunge kabla ya kupitisha fedha, hivyo ni ishara kuwa Bunge si dhaifu kwa sababu wamefanikisha suala hilo. Ameongeza: "Wakati bajeti inapitishwa kulikuwa na mjadala mkali kwa sababu wabunge walikuwa wanahitaji kujua kwa nini kodi inayotokana na matumizi ya simu ni ndogo kuliko idadi ya watumiaji wa simu.” 

Mvutano kati ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu na Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad na Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai uliibuka baada ya CAG kuitwa na Spika wa Bunge kufika bungeni kwake ili ahojiwe kufuatia kauli yake ya kukitaja chombo hicho kwamba ni dhaifu. Viongozi wa upinzani na wanasheria wameitaja hatua hiyo ya Ndugai kuwa inakiuka katiba ya nchi hiyo mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Tags

Maoni