Feb 06, 2019 07:30 UTC
  • Watu 9 wauawa katika wimbi jipya la mapigano Sudan Kusini

Kwa akali watu tisa wameripotiwa kuuawa katika wimbi jipya la mapigano katika jimbo la Amadi, magharibi mwa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa jana na Manasseh Dobuyi, Naibu Gavana wa jimbo la Amadi, askari saba na raia wawili waliuawa katika mapigano hayo ya mwishoni mwa wiki kati ya askari watiifu kwa kiongozi wa upinzani Riek Machar (SPLM-IO) na wapiganaji wa National Salvation Front (NAS) inayoongozwa na Jenerali Thomas Cirillo.

Jenerali Cirillo alikataa kusaini makubaliano ya amani kati ya serikali na makundi ya waasi mjini Addis Ababa Ethiopia mwaka jana. Macahar anatazamiwa kuelekea Juba mwezi Mei mwaka huu kwa ajili ya kuanza kutekeleza mapatano hayo.

Haya yanajiri siku chache baada ya Jumuiya ya Maendeleo ya Serikali ya Nchi za Afrika Mashariki IGAD kubainisha masikitiko yake kuhusu ukiukaji wa mapatano ya amani yaliyosainiwa Septemba mwaka 2018, kati ya serikali ya Sudan Kusini na makundi ya waasi.

Rais Kiir na Machar katika kikao na mpatanishi, Rais Omar al-Bashir wa Sudan

Mapigano ya ndani nchini Sudan Kusini yalianza tarehe 15 Disemba 2013 baada ya Rais Salva Kiir kumfuta kazi makamu wake wakati huo Riek Machar kwa madai kuwa alipanga njama ya kumpindua.

Hadi hivi sasa watu laki tatu na 85 elfu wameshauawa na mamilioni ya wengine wamejeruhiwa na kuwa wakimbizi.

Tags

Maoni