Feb 16, 2019 15:10 UTC
  • Ripoti: Wanawake wakiwemo wajawazito walilengwa katika ukatili wa kingono Sudan Kusini

Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa jana imeripoti ongezeko la ukatili wa kingono katika jimbo la Unity la kaskazini mwa Sudan Kusini.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa, wanawake na wasichana 134 wamebakwa na wengine 41 wamekabiliwa na aina nyingine ya ukatili wa kingono kati ya Septemba na Disemba mwaka jana.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva huko Uswisi, msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, Rupert Colville amesema kuwa, “asilimia 87 ya wanawake na wasichana walibakwa na zaidi ya mtu mmoja  kwa saa nyingi. Miongoni mwa watu waliobakwa, 50 walikuwa watoto huku mtoto mmoja akiwa na umri wa miaka minane, wanawake wajawazito na wanawake wanaonyonyesha pia walilengwa na ukatili huo.

Amesema kuwa, katika kisa kimoja Disemba 17 mwaka jana huko kwenye kijiji cha Langa kaskazini mwa Bentiu, wanawake watano walibakwa ambapo wanne kati yao walikuwa na ujauzito, mmoja wao akiwa na ujauzito wa karibu miezi tisa na mwingine miezi saba.

Ripoti ya Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imeeleza kwamba, uchunguzi uliofanyika unaonyesha kuwa, kuna mambo mbalimbali yaliyochangai hali hiyo. Wakati huo huo,

Michelle Bachelet Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito kwa mamlaka nchini Sudan Kusini kuchukua hatua ikiwemo zilizoorodheshwa kwenye makubaliano ya amani, kulinda wanawake na wasichana, kuchunguza kwa haraka madai ya ukatili wa kingono na kuwawajibisha wahusika kwa mujibu wa sheria.

Maoni