Feb 21, 2019 08:03 UTC
  • Jenerali Ulimwengu: Rais Magufuli ana uthubutu, lakini asikilize anayoambiwa na watu

Jenerali Ulimwengu, mwandishi mkongwe wa habari na mkosoaji mashuhuri wa serikali nchini Tanzania sambamba na kumuunga mkono Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania, amemtaka rais huyo kusikiliza yale anayoambiwa na wananchi.

Ulimwengu ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza katika kongamano la ‘Wenye Nchi ni Wananchi’ lililoandaliwa na Jukwaa la Tanzania Yenye Mabadiliko, ambapo akipongeza hatua mbalimbali zinazotekelezwa na rais huyo za kuwaletea maendeleo wananchi amemshauri kuwafungulia milango  watu kwa ajili ya kuhoji na kutoa mawazo yao mbadala kuhusiana na uwajibikaji na utekelezaji wa masuala yanayohusu maendeleo ya nchi yao.  “Huwa sipendi sana kumsifu (Rais Magufuli) lakini kuna mambo mengi sana ambayo amefanya kwa uthubutu, wakati mwingine anakosea, lakini anathubutu angalau, anachohitaji ni kusikiliza zaidi watu wanamwambia nini pale ambapo tunadhani amekosea,”  amesema Jenerali Ulimwengu.

Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania

Aidha amewataka viongozi wa serikali kuwa waaminifu badala ya kuwa watiifu na kubainisha kwamba, uaminifu ndio jambo muhimu katika utendajikazi badala ya utiifu ambao mara nyingi humfanya muhusika kutii kila kitu anachoamrishwa hata kama kitakuwa kibaya. "Wewe huna la kusema, basi tu kwa kuwa umepewa maelekezo kutoka juu? unatenda tu hata kama unaamini kwamba unachokitenda ni kosa?" Kadhalika Jenerali Ulimwengu ambaye mara nyingi amekuwa akikosoa serikali nchini Tanzania ameenda mbali na kusema kuwa, baada ya kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia, viongozi wa Manazi waliohusika na mauaji katika vita hiyo walipandishwa kizimbani (Nuremberg trials) ambapo walijitetea kuwa walitenda jinai hizo kwa sababu walipewa amri kutoka juu, na kwamba utetezi wao huo haukuzingatiwa.“Watu wanayo nia njema ya kumsaidia Rais lakini wakati mwingine anaonekana kama hasikilizi sawasawa, lakini angalau kwa uthubutu anao.” Amesema Ulimwengu.

Tags

Maoni