Mar 04, 2019 14:52 UTC
  • Rais Magufuli aliambia Jeshi la Polisi kuwa, kuna maswali mengi kuhusu sakata la kutekwa Mohammed Dewji

Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania, amesema kuwa, suala la kutekwa nyara kwa mfanyabiashara mashuhuri wa nchi hiyo na Afrika, Mohammed Dewji mashuhuri kwa jina ‘Mo’ limeacha maswali mengi kwa wananchi ambayo yanahitaji majibu hivyo jeshi la polisi liwaeleze Watanzania kwani si wajinga sana.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo mara baada ya kuwaapisha mawaziri wapya wa Katiba na Sheria, Balozi Agustine Mahiga na wa Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, ambapo amesema ana imani kubwa na jeshi la polisi lakini kuna dosari zinazopaswa kufanyiwa kazi huku akitolea mfano wa tukio la kutekwa nyara kwa mfanyabiashara huyo. Ameongeza kuwa, Watanzania wanajua kuchambua mambo na lilipotokea tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara huyo ziliibuka habari nyingi kwamba waliohusika na utekaji ni Wazungu wa aina fulani lakini suala hilo lilipomalizika liliacha maswali mengi zaidi. “Mtu aliyetekwa alikutwa Gymkhana usiku lakini watu wanajiuliza Mmhh aliendaje pale, lakini alipowekwa pale na bunduki zikaachwa pale, unajiuliza huyu mtekaji aliyeamua kuziacha je angekutana na polisi wanaotafuta njiani?” Amehoji Rais Magufuli.

Tarehe 20 Oktoba 2018 siku aliyopatikana mfanyabiashara huyo

Amezidi kubainisha kwamba, siku chache baada ya tukio hilo Watanzania walionyeshwa nyumba alipokuwa ameshikiliwa ndani yake kama ambavyo pia walionyeshwa na aliyekuwa akiwabeba wale watekaji, lakini tangu wakati huo hakuna kilichoendelea licha ya kusubiria kwa hamu kuona kwamba mtu huyo angepelekwa mahakamani na nini kingetoa baadaye. Rais John Pombe Magufuli amesema kuwa, jambo hilo linaaacha maswali mengi ambayo hayana majibu, mtu aliyekuwa akiwasafirisha angewataja na Watanzania walitaka kuona huyo mmiliki wa nyumba angalau akajibu. “Haya hata kama Watanzania watanyamaza lakini mioyo yao haitakuwa clear (safi).” Amesema. Itakumbukwa kuwa, Mohammed Dewji alitekwa nyara Oktoba 11, mwaka jana majira ya saa 11 alfajiri eneo la Hotel ya Colosseum iliyopo barabara ya Haile Selassie, Oysterbay jijini Dar es Salaam ambako alikwenda kufanya mazoezi na akapatikana Oktoba 20 eneo la Gymkhana jijini hapo.

Tags

Maoni