Mar 18, 2019 15:05 UTC
  • Chadema yampongeza Maalim Seif, awataka wafuasi wake wasitetereke, waungane naye ACT-Wazalendo huko Tanzania

Mwanasiasa maarufu nchini Tanzania na Afrika Mashriki kiujumla, Maalim Seif Sharif Hamad leo Jumatatu, tarehe 18 Machi, 2019, ametangaza rasmi mbele ya waandishi wa habari kukihama Chama cha Wananchi CUF na kujiunga na cha chama cha ACT-Wazalendo cha Zitto Zuberi Kabwe. Amesema kuwa yeye, viongozi, pamoja na wafuasi wanaomuunga mkono wa visiwani Zanzibar na Tanzania Bara wamehamia rasmi katika Chama cha ACT-Wazalendo.

Wakati hayo yakijiri, Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk Vincent Mashinji amempongeza Maalim Seif Sharif Hamad kwa uamuzi wake wa  kujiunga na Chama cha ACT- Wazalendo na kusema uamuzi wake ni sahihi.

Maalim Seif ametangaza uamuzi huo zikiwa zimepita saa chache tangu Mahakama Kuu ya Tanzania kuhalalisha uenyekiti wa Profesa Ibrahim Lipumba ndani ya CUF hali iliyomuweka kando Maalim Seif.

Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Tanzania, kutangaza kuihama CUF na kujiunga na ACT-Wazalend. Jumatatu, Machi 18, 2019.

Kwa muda mrefu chama cha CUF kilikuwa kinazilalamikia mamlaka za Tanzania kwa kuingilia masuala ya ndani ya chama hicho hasa hatua ya msajili wa vyama ya kumtambua Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti wa chama hicho licha ya kwamba aliandika barua rasmi ya kujiuzulu uenyekiti wa CUF.

Akizungumza na waandishi wa habari leo mchana katika ofisi za wabunge wa CUF Magomeni jijini Dar es Salaam, Maalim Seif amesema mapambano ya kisiasa lazima yaendelee.

Viongozi wakuu wapya wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Zuberri Kabwe na Maalim Seif Shariff Hamad

 

Katika sehemu moja ya taarifa yake kwa vyombo vya habari, Maalim Seif amesema: Tunahitaji JAHAZI la kutufikisha kwenye TANZANIA MPYA inayoheshimu utu, ubinadamu, haki na yenye neema inayofika kwa wananchi wote. Jahazi hilo ni ACT-WAZALENDO. Vile vile amesema: "Hatua tunayochukua leo ni kuandika historia mpya ya mabadiliko ya kisiasa Tanzania, kote Zanzibar na Bara." Aidha amesema: "Umma haujawahi kushindwa popote duniani. Ndivyo historia inavyoonesha."

 

Maoni