Mar 19, 2019 16:33 UTC
  • Siasa za upinzani TZ zazidi kunoga; Maalim Seif akabidhiwa kadi namba moja ya uwanachama ACT-Wazalendo

Siasa za upinzani TZ zazidi kunoga, baada ya Maalim Seif kukabidhiwa kadi namba moja ya uwanachama ACT Wazalendo

Mwanasiasa mkongwe katika siasa za upinzani nchini Tanzania Maalim Seif Sharif Hamad, leo amejiunga rasmi na chama cha upinzani cha ACT- Wazalendo, siku moja baada ya kutangaza kukihama chama cha upinzani cha Wananchi CUF.

Maalim Seif, ambaye alikuwa mmoja wa waasisi wa CUF na Katibu Mkuu wa muda wa mrefu wa chama hicho, amekabidhiwa kadi namba moja ya uwanachama wa chama cha ACT- Wazalendo, ambayo imeshalipiwa kwa muda wa miaka 10, na kiongozi wa chama hicho Zitto Zuberi Kabwe katika hafla maalumu iliyofanyika makao makuu ya chama hicho Mwananyamala jijini Dar es Salaam.

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe (kushoto) akimkabidhi Maalim Seif Sharif Hamad kadi ya uwanachama wa chama hicho

Mbali na Maalim Seif mwenyewe, viongozi wengine wa kambi ya kiongozi huyo kutoka chama alichokihama cha CUF ambao wamekabidhiwa kadi za uwanachama ACT-Wazalendo ni Ismail Jussa, Mbalala Maharangande, Sheweji Mketo na mmoja wa wanasiasa machachari,  Juma Duni Haji, ambaye amekabidhiwa kadi namba kumi.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa kadi yake ya uwanachama, Maalim Seif, amesema yeye ni mara ya kwanza kukanyaga ofisi za ACT- Wazalendo lakini anajiona ni mwenyeji.

Maalim Seif Sharif Hamad akilakiwa na wanachama wa CUF wakati alipkuwa Katibu Mkuu wa chama hicho

Wakati huohuo Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Tanzania Jaji Francis Mutungi amekemea kile alichoeleza kuwa ni vitendo vya uvunjifu wa sheria ambavyo amesema vinafanywa na baadhi ya wanachama wa  Cuf wanaomuunga mkono aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.

Katika taarifa rasmi aliyotoa kwa umma hii leo, Mutungi amesema, kumezuka vitendo vya uvunjifu wa sheria  ikiwemo kuchoma moto bendera za chama cha CUF vinavyofanywa na mashbiki wa Maalim Seif.

Amesisitiza kuwa sheria ya vyama vya siasa inakataza kitendo chochote kinachodhihaki bendera ya chama cha siasa na kuonya kuwa watakaofanya hivyo watachukuliwa hatua wao wenyewe pamoja na vyama vyao.

Msajili wa vyama vya siasa Tanzania, Jaji Francis Mutungi

Msajili huyo wa vyama vya siasa Tanzania amekemea pia kile alichokitaja kama kutumiwa dini na vyama vya siasa kwa ajili ya kufikia malengo yao.

Tangu Maalim Seif Sharif Hamad alipotangaza kujiunga na chama cha ACT-Wazalendo hapo jana, kumekuwa kukishuhudiwa video katika mitandao ya kijamii za watu wanaoaminika kuwa wafuasi wa kiongozi huyo, wakichoma moto bendera za chama cha CUF na baadhi yao wakipandisha bendera ya chama cha ACT-Wazalendo huku wakitoa takbira.../  

 

Tags

Maoni