Mar 20, 2019 16:47 UTC
  • Chadema Tanzania: Tulitamani kumchukua Maalim Seif, lakini hatukufikia mwafaka

Chama cha Demokrasia na Maendeleo nchini Tanzania Chadema ambacho ni chama kikuu cha upinzani nchini humo, kimesema kuwa, kilitamani kumchukua aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, lakini hakikufikia makubaliano na mwanasiasa huyo.

Taarifa iliyotolewa na chama hicho kupitia Salum  Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu Chadema Zanzibar imesema kuwa,pamoja na hali hiyo kimeweka azma ya kushirikiana na Maalim Seif katika chama chake kipya cha ACT Wazalendo. Mwalimu ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam, na kuongeza kwamba licha ya kumkosa Maalim Seif na kundi lake wataendelea kushirikiana naye kwa kuzingatia mkutano wa vyama vya upinzani uliofanyika Zanzibar Desemba 2018. "Hakuna pigo, tulimtaka kweli. Viongozi wetu kwa hekima na busara waliona huyu mtu akija huku ni jambo jema na sisi tuliona tunusuru hadhi na heshima yake na mapambano ya demokrasia." Aidha mwishoni mwa mwaka jana, Baraza la Wazee la Chadema lilitoa tamko la kumkaribisha Maalim Seif kwenye chama hicho wakati mgogoro wa CUF ulipokuwa ukiendelea.

Mgogoro uliokuwa ukiendelea kati ya Maalim Seif na Lipumba

Kuhusu nguvu ya Chadema Zanzibar, Mwalimu amesema chama hicho kitaendelea na programu zake visiwani humo, lakini hakitapambana na ACT-Wazalendo. Maalim Seif Sharif Hamad alikuwa mmoja wa wanasiasa waliounga mkono kwa nguvu zote uamuzi wa vyama vinne vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kumuunga mkono Edward Lowassa aliyeteuliwa na Chadema kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 nchini Tanzania. Msimamo wake huo ndio uliomfanya mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kujiuzulu wadhifa wa mwenyekiti taifa wa chama, lakini akarejea tena takriban miezi minane baadaye akitaka arejeshewe madaraka yake ya zamani, hali iliyoibua mgogoro ulioishia mahakamani na baadaye Maalim Seif na wafuasi wake kushindwa kesi na kuamua kujiondoa na kujiunga chama cha ACT-Wazalendo ambacho hakikuwamo kwenye umoja wa Ukawa wala hakikumuunga mkono Lowassa katika uchaguzi mkuu uliopita.

 

 

 

 

Tags

Maoni