Mar 22, 2019 01:17 UTC
  • UN: DRC inahitaji dola bilioni 1.6 kwa ajili ya misaada ya kibinadamu

Umoja wa Mataifa umesema unahitaji msaada wa dola bilioni 1.65 za Marekani kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya msingi na ya kibinadamu ya watu milioni 9 wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, walioathiriwa na mapigano.

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa Unicef, Henrietta Fore na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura, Mark Lowcock wamesema ingawaje hali katika nchi hiyo kubwa ya katikati mwa Afrika inazidi kuimarika, lakini misaada hiyo ya kibinadamu itaendelea kuhitajika hadi pale taifa hilo litakapopata amani ya kudumu.

Unicef imesema inahitaji dola milioni 326 ili kushughulikia mahitaji ya kibinadamu ya watoto milioni 4.3 wa nchi hiyo ambao inasema wapo katika mgogoro mkubwa.

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa umesema kuwa, licha ya hatua kubwa kupigwa katika miaka ya hivi karibuni ikiwemo kupungua idadi ya watoto wadogo wanaofariki dunia kabla ya miaka mitano na ongezeko la watoto kujiunga na shule, lakini kwa ujumla hali ya kibinadamu Kongo DR ni ya kutia wasiwasi.

Watoto ndio wahanga wakuu wa mgogoro na mapigano DRC

Shirika hilo la kushughulikia masuala ya watoto la UN limebainisha kuwa, idadi ya watu wanaokabiliwa na baa la njaa nchini humo iliongezeka kutoka watu milioni 7.7 mwaka 2017 hadi watu milioni 13 mwaka jana 2018.

Kwa mujibu wa Unicef, watoto milioni nne wa DRC wanakabiliwa na utapiamlo, huku magonjwa ya kipindupindu, surua na Ebola yakiendelea kutishia maisha ya idadi kubwa ya watu wa nchi hiyo ya Kiafrika, yenye utajiri wa madini.

 

 

Tags

Maoni