Mar 25, 2019 08:02 UTC
  • Rais wa Mali awapiga kalamu nyekundu makamanda wawili wa jeshi kufuatia mauaji ya watu 134

Kufuatia kushtadi vitendo vya ukatili nchini Mali na pia kuuawa watu 134 wa eneo la Fulani na wabeba silaha, Rais Ibrahim Boubacar Keïta wa nchi hiyo amempiga kalamu nyekundu mkuu wa majeshi na kamanda wa kikosi cha ardhini nchini.

Mauaji hayo yametokea katika kipindi kilicho chini ya wiki moja baada ya kutokea shambulizi la kigaidi dhidi ya kambi moja ya kijeshi lililosababisha jumla ya askari 23 kuuawa. Kundi moja la kigaidi na ukufurishaji lenye mahusiano na genge la al-Qaidah lilitangaza kuhusika na shambulizi hilo. Raia wa Mali wamekuwa wakilalamikia udhaifu wa jeshi la nchi hiyo na wamelitaka lidhibiti vitendo vya jinai na mauaji na pia kuwalinda.

Sehemu ndogo ya jinai zilizofanywa na makundi ya wabeba silaha dhidi ya wanavijiji nchini Mali

Miongoni mwa jinai ambazo zimefanywa nchini Mali na makundi ya wabeba silaha ni pamoja na mauaji ya wanawake na watoto wa vijiji viwili yaliyotokea hivi karibuni ambapo katika jinai hiyo ya kinyama miili ya wahanga hao ilichomwa moto na washambuliaji. Licha ya askari 4500 wa Kifarasa kuwepo katika eneo la Sahel mwa Afrika, lakini mashambulizi ya kigaidi yameshika kasi katika eneo hilo. Askari hao wa kigeni walifika eneo hilo mwaka 2013 kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi. Weledi wa mambo wanaamini kwamba uwepo wa askari wa madola ya Magharibi katika eneo hilo, ndio sababu ya kushtadi jinai za makundi ya kigaidi.

Maoni