Mar 26, 2019 07:34 UTC
  • Sheikh Zakzaky ashindwa kufika mahakamani kutokana na hali mbaya ya kiafya

Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, Sheikh Ibrahim Zakzaky ameshindwa kufika mahakamani kutokana na kudorora hali yake ya afya.

Wakili wa Sheikh Zakzaky amesema kiongozi huyo wa kidini nchini Nigeria anahitaji huduma ya dharura ya afya na kwamba hali yake imezidi kudhoofu. Amesema mwanahakarati huyo wa Kiislamu nchini Nigeria ameshindwa kwenda mahakamani kusikiliza kesi yake, na kwa msingi huo kikao cha kesi hiyo kimeakhirishwa kwa muda usiojulikana.

Mahakama nchini Nigeria imekataa kumwachia huru kwa dhamana kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya nchini humo, licha ya hali yake ya afya na licha ya maandamano ambayo hufanyika mara kwa mara kushinikiza kuachiwa huru kiongozi huyo wa kidini.

Mahakama Kuu ya jimbo la Kaduna kaskazini mwa Nigeria ilidai kuwa hakuna ushahidi wa maana uliowasilishwa mahakamani ili kuweza kumwachia kwa dhamana Sheikh Ibrahim Zakzaky.

Sheikh Zakzaky alipofikishwa mahakamani mwaka uliopita

Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe walikamatwa na kuwekwa kizuizini tarehe 13 Desemba 2015, wakati askari wa jeshi la Nigeria walipovamia na kufanya hujuma dhidi ya Hussainiyyah ya mji wa Zaria katika jimbo la Kaduna kaskazini mwa nchi hiyo, ambapo mamia ya Waislamu waliuawa shahidi.

Mnamo mwezi Desemba 2016, Mahakama Kuu ya Nigeria ilitoa hukumu ya kutaka Sheikh Zakzaky aachiwe huru mara moja, sambamba na kulitaka jeshi na vyombo vya usalama viilipe familia yake fidia ya dola laki moja na nusu, lakini si tu vimekaidi kutekeleza hukumu hiyo ya mahakama lakini vimeendelea pia kumweka kizuizini kiongozi huyo wa kidini pamoja na mkewe.

Tags

Maoni