Mar 26, 2019 07:35 UTC
  • Waziri: Hakuna mgogoro wa kisiasa Sudan, yaliyoko ni matatizo ya kiuchumi

Waziri wa Habari wa Sudan amesema hakuna mgogoro wa kisiasa katika nchi hiyo, bali kinachoshuhudiwa ni changamoto za kiuchumi.

Hassan Ismail ameyasema hayo katika mahojiano na shirika la habari la Reuters na kufafanua kuwa, nchi hiyo haikabiliwi na mgogoro wowote wa kisiasa kama ambavyo imekuwa ikiripotiwa na vyombo vya habari vya ndani ya nje ya nchi na kwamba maandamano ya wananchi ni ya kulalamikia matatizo ya kiuchumi.

Kadhalika amekanusha madai kwamba serikali inavikandamiza vyombo vya habari na mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini humo na kubainisha kuwa, "Nchi hii ina uhuru wa vyombo vya habari, magazeti ya wapinzani yanauzwa mjini Khartoum, na pia haki ya wananchi ya kuandamana imeainishwa kwenye katiba."

Hii ni katika hali ambayo, jana Jumatatu makumi ya wanahabari waliandamana katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum wakitaka kuachiliwa huru Osman Mirghani, Mhariri Mkuu wa gazeti mashuhuri la al-Tayar sambamba na kulalamikia ukandamizaji wa vyombo vya usalama dhidi ya waandamanaji.

Rais wa Sudan

Maandamano ya hivi sasa ya nchini Sudan ni makubwa zaidi kuwahi kuikumba nchi hiyo katika kipindi cha miaka 30 iliyopita, ambapo watu zaidi ya 50 wameuawa katika ghasia na maandamano hayo.

Maandamano hayo yaliyoanza kwa kulalamikia ughali wa maisha yamebadilika na kuwa wimbi la kumtaka Rais Omar al Bashir wa nchi hiyo ang'oke madarakani, lakini bado anashikilia msimamo wake wa kubakia uongozini.

Tags

Maoni