Apr 23, 2019 14:20 UTC
  • Serikali ya Tanzania: Hatujazuia kuchapishwa ripoti ya IMF, bado tunafanya majadiliano nao

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema kuwa bado inaendelea kufanya majadiliano na Shirika la Fedha Duniani (IMF) kuhusiana na ripoti ya hivi karibuni ya shirika hilo kuulenga uchumi wa nchi hiyo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango wakati akijibu swali la mbunge wa Tunduma wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Frank Mwakajoka na kuongeza kwamba serikali ya Dar es Salaam, haijazuia kuchapishwa ripoti hiyo bali inaendelea na mazungumzo na IMF. Kauli hiyo imekuja ikiwa ni wiki moja tangu Shirika la Fedha Duniani (IMF) kueleza kuwa limezuiwa kuchapisha taarifa ya tathmini ya uchumi wa Tanzania, suala ambalo limekanushwa na serikali ya nchi hiyo mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Awali mbunge huyo wa upinzani alikuwa amehoji ni kwa nini Tanzania imezuia uchapishaji wa taarifa hiyo.

Shirika la Fedha Duniani (IMF)

Katika taarifa yake Shirika hilo la Fedha Duniani liliitangazia dunia kuwa, serikali ya Tanzania, imezuia kuchapishwa tathmini iliyofanywa na pia kutolewa taarifa kwa vyombo vya habari. Aidha ripoti hiyo ilisema kuwa, licha ya Rais John Magufuli wa Tanzania kutekeleza mpango wa kuimarisha viwanda nchini humo lakini uwekezaji wa kigeni umepungua nchini humo kutokana na sera za serikali kuingilia sekta za uchimbaji madini na kilimo, suala ambalo litadhoofisha uchumi wake. Baada ya taarifa hiyo fupi, vyombo vya habari vya kimataifa viliripoti baadhi ya wanasiasa pamoja na wanaharakati kujitokeza wakitaka taarifa iwekwe wazi ili wananchi wajue mwenendo wa uchumi wa nchi yao.

Tags

Maoni