Apr 24, 2019 03:39 UTC
  • Nafasi ya Saudia na Imarati kabla na baada ya kupinduliwa serikali ya al-Bashiri nchini Sudan

Baada ya maandamano ya miezi sita, hatimaye utawala wa miaka 30 wa Rais Omar al-Bashiri wa Sudan uling'olewa madarakani na jeshi la nchi hiyo mnamo tarehe 11 Aprili mwaka huu.

Omar al-Bashir aliingia madarakani mwezi Juni 1989 kupitia mapinduzi yasiyo ya umwagaji damu na hatimaye kuwekwa pembeni na jeshi tarehe 11 Aprili baada ya maandamano ya wananchi yaliyoandamana na ghasia,  yaliyoanza tarehe 19 Disemba mwaka uliopita wa 2018 na kupelekea zaidi ya watu 50 kuuawa. Saudi Arabia na Imarati ni nchi mbili za Kiarabu ambazo zimetumia fedha nyingi kumbakisha madarakani Bashir lakini nguvu ya wananchi wa Sudan imekuwa na uwezo mkubwa kuliko dola za nchi hizo.

Katika hatua ya pili na baada ya kushindwa Saudia na Imarati kumlinda al-Bashir, nchi mbili hizo zimetumia vyombo vya intelijensia vya utawala haramu wa Israel kumuondoa madarakani kiongozi huyo wa zamani wa Sudan. Hii ni katika hali ambayo Bashir alituma idadi kubwa ya askari wa Sudan kushiriki katika hujuma ya kichokozi ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia dhidi ya Yemen. Katika hatua ya tatu baada ya kung'olewa madarakani al-Bashir nchi  hizo sasa zinashirikiana kwa karibu na Marekani kwa ajili ya kuongoza na kuelekeza matukio ya nchi hiyo ya Kiafrika katika mkondo zinaoutaka.

Omar al-Bashir (kushoto) aliyesalitiwa na watawala wa Saudia

Ni kwa msingi huo ndipo Abdulfattah al-Burhan, kamanda wa jeshi la nchi kavu la Sudan ambaye ana nafasi muhimu katika vita vya Yemen na ambaye pia ana uhusiano mzuri na wa karibu na Riyadh na vilevile Abu Dhabi akapewa jukumu la kuongoza Baraza Kuu la Kijeshi la Mpito la Sudan linalosimamia kwa sasa mambo ya nchi hiyo. Katika kipindi hiki Saudia na Imarati zinatumia fedha nyingi kwa ajili ya kulinda na kuimarisha nafasi ya wanajeshi wafanyamapinduzi na hasa ya Abdulfattah al-Burhan nchini Sudan. Tayari zimetoa dola bilioni 3 kwa lengo hilo ambapo dola miolioni 500 kati ya hizo zinatumika katika Benki Kuu ya Sudan kwa madhumuni ya kuimarisha shughuli zake za kifedha. Msaada huo wa fedha umetolewa kwa kisingizio kwamba utaweza kuzima malalamiko ya wananchi wa Sudan ambayo inadaiwa yametokana na masuala ya kiuchumi. Kuhusu hilo, shirika rasmi la habari la Saudia limesema: 'Msaada huo umetolewa kwa ajili ya kuimarisha hali ya kifedha ya Sudan, kuleta uthabiti katika soko la fedha za kigeni na vilevile kuboresha hali jumla ya uchumi wa nchi hiyo.'

Lengo la Saudi Arabia na Imarati katika hatua hii ni kuzuia kukamilika kwa mapinduzi ya wananchi wa Sudan kama ilivyofanyika kuhusiana na  mapinduzi ya watu wa Misri na Yemen. Riyadh na Abu Dhabi zinataka kutekeleza huko Sudan njama ziliyotekeleza Misri kwa kuwaweka madarakani wanajeshi ambao watakuwa wakitii na kutekeleza kikamilifu amri zao.

Abdulfattah al-Burhan, kiongozi wa kijeshi wa hivi sasa wa Sudan

Nchi mbili hizo za Kiarabu ambazo zina rekodi mbaya ya kuingila mambo ya ndani ya nchi nyingine za Kiarabu zinalipa kipaumbele suala la kuunga mkono Baraza Kuu la Kijeshi la Mpito nchini Sudan. Kuhusiana na suala hilo Baraza la Kifalme la Saudia limetoa taarifa likiutaja uhusiano wa hivi sasa wa nchi hiyo na Sudan kuwa wa kihistoria na kusema: 'Riyadh inafuatilia matukio ya Sudan na taarifa za Baraza Kuu la Kijeshi la Mpito, na kutangaza uungaji mkono wake kwa hatua za baraza hilo.'

Wizara ya Mambo ya Nje ya Imarati pia bila kupoteza wakati imetoa taarifa ikiyataja matukio ya Sudan kuwa ya kihistoria na kupongeza kuteuliwa kwa Abdulfattah al-Burhan kuwa mkuu wa Baraza Kuu la Kijeshi la Mpito. Imesisitiza kwamba ina imani kamili juu ya nguvu ya wananchi na jeshi la Sudan kwa ajili ya kuvuka vitisho vilivyopo.

Maoni