Apr 24, 2019 06:28 UTC
  • Libya katika kinamasi cha mapigano ya ndani na uingiliaji wa madola ajnabi

Mapigano nchini Libya hasa katika mji wa Tripoli na pambizoni mwake yanakuwa makali siku baada ya siku. Duru za kijeshi za Serikali ya Umoja wa Kitaifa zimetangaza kuwa, vikosi vyake vimefanikiwa kudhibiti sehemu kubwa ya uwanja wa ndege wa Tripoli. Hata hivyo wapiganaji wa Jenerali Khalifa Haftar wamedai kuwa wamekaribia mno kuingia katikati ya Tripoli.

Mgogoro wa Libya iliingia katika hatua mpya tangu mwanzoni mwa mwezi huu wa Aprili. Wakati jamii ya kimataifa ilipokuwa mbioni kuandaa kikao maalumu cha kuutafutia ufumbuzi wa kisisa mgogoro wa Libya na kuandaa mazingira mazuri ya kufanyika uchaguzi mkuu, Jenerali Khalifa Haftar alivuruga mipango yote hiyo ya jamii ya kimataifa kwa hatua yake ya kuushambulia mji mkuu Tripoli, hapo tarehe 4 Aprili, 2019. 

Siku 20 zimepita tangu jenerali huyo anayeungwa mkono na Saudi Arabia, rais wa Marekani, Donald Trump, Misri, rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) alipoanzisha vita dhidi ya Tripoli. Jenerali Haftar alianzisha vita dhidi ya Tripoli kwa tamaa ya kuuteka haraka mji huo lakini muqawama wa wanajeshi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa umebatilisha ndoto yake hiyo.

Madola ajinabi hayajali madhara linayopata taifa la Libya, yanachonganisha makundi hasimu ili kudhamini maslahi yao ya kibeberu

 

Pamoja na hayo mashambulizi hayo mapya dhidi ya mji mkuu wa Libya yameshasababisha maafa makubwa ya roho za watu na mali. Shirika la Afya Dunia (WHO) limetangaza kuwa, zaidi ya watu 450 wameuawa na kujeruhiwa katika kipindi hiki cha siku 20 na zaidi ya wat 20 elfu wengine wamekuwa wakimbizi. 

Katika upande wa kidiplomasia pia, dunia inashuhudia mgawanyiko kuhusu Libya na mgogoro wake. Nchi nyingi za Ulaya bado zinaiunga mkono Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na Fayez al Sarraj na zinasisitiza kuwa hiyo ndiyo serikali halali nchini Libya. Nchi hizo zinasema utatuzi wa mgogoro wa Libya si wa kijeshi.

Waziri Mkuu wa Italia, Giuseppe Conte amesema, hakuna manufaa yoyote ya kiuchumi au ya kiistratijia yanayoweza kuhalalisha vita vya ndani nchini Libya na kuongeza kuwa: Ni wajibu wetu kufanya juhudi zetu zote kuhakikisha hakutokei mgogoro wa kibinadamu nchini Libya kwani iwapo mgogoro huo utatokea si tu madhara yake yatakuwa makubwa kwa Italia na bara zima la Ulaya, lakini pia wananchi wa Libya nao watakumbwa na hali ngumu sana.

Katika upande mwingine, wachambuzi wengi wa masuala ya kijeshi wanaamini kuwa, Jenerali Khalifa Haftar ameanzisha mashambulizi dhidi ya mji wa Tripoli kwa baraka kamili za Marekani na kwa uungaji mkono wa kifedha wa Saudi Arabia na Imarati.

Jenerali Khalifa Haftar alianzisha mashambulizi dhidi ya Tripoli, Libya Aprili 4, 2019 baada ya kutembelea Saudia na mara baada ya kuzungumza kwa simu na rais wa Marekani, Donald Trump

 

Jeffrey D. Feltman amemlaumu vikali Donald Trump kwa uungaji mkono wake kwa Jenerali Khalifa Haftar na kusema kuwa uungaji mkono huo ndio uliopelekea jenerali huyo kuanza kuushambulia kikolela mji wa Tripoli. Amesema: Si sadfa kuona mashambulizi ya kiholela yalianzishwa na Jenerali Khalifa Hafatr mara tu baada ya kuzungumza kwa simu na Trump.

Mapigano nchini Libya yanaendelea kwa nguvu zote katika hali ambayo, nchi hiyo inaonekana kuwa imegeuzwa uwanja wa kulipiziana kisasi nchi tofauti ajinabi ambazo hazijali kabisa matakwa na matumaini ya wananchi wa Libya ya kuwa na nchi yenye utulivu inayoendeshwa kidemokrasia.

Wananchi wengi wa Libya wana wasiwasi kwamba iwapo Jenerali Khalifa Haftar atashinda vita hivyo basi ataiongoza Libya kwa udikteta mkubwa dhidi ya wanchi sambamba na kuwa kibaraka mkubwa wa madola ya kigeni.

Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, njia pekee ya kuliokoa taifa la Libya ni kukomeshwa haraka uingiliaji wa madola ya kigeni, kukomeshwa vita na kuenedelea na mazungumzo ya kutatua kisiasa masuala ya nchi hiyo kwa kushirikishwa makundi yote ya Libya na kuielekeza nchi hiyo upande wa utulivu wa kudumu wa kisiasa.

Tags

Maoni