Apr 24, 2019 07:50 UTC
  • Mafuriko yaua zaidi ya 50 nchini Afrika Kusini

Mafuriko na mmomonyoko wa udongo umepelekea watu wasiopungua 51 kupoteza maisha katika mkoa wa KwaZulu-Natal, mashariki mwa Afrika Kusini.

Maafa hayo yamesababishwa na mvua kubwa ambazo zinaendelea kunyesha katika mkoa huo tokea siku ya Jumatatu. Mafuriko hayo pia yameharibu maeneo mengi ya makazi pamoja na maelfu ya hekari za ardhi ya kilomo.

Kiwango cha maji kimekuwa kikiongezeka katika mkoa huo na kuwalazimisha baadhi ya wakazi wa viunga vya mji wa Durban ulioko kwenye mkoa huo kuyahama makazi yao.

Ripoti zinasema kuwa miili ya wahanga wa mafuriko hayo inaendelea kuopolewa kutoka kwenye maji ya mafuriko ambayo hadi sasa yamewasababishia wakazi wa maeneo yaliyoathirika maafa na hasara kubwa.

Uharibifu unaosababishwa na mafuriko

Waokoaji wanafanya kila wanaloweza kuokoa na kuwahamishia maeneo salama wahanga ambao bado wako kwenye maeneo hatari na yasiyofikika kirahisi.

Licha ya hasara iliyopatikana lakini watabiri wa hali ya hewa wanasema kuwa hakuna dalili yoyote ya kupungua mvua hizo na kwamba mvua zaidi zinatarajiwa kunyesha katika eneo hilo siku chache zijazo. Kinyume na mvua zilizoshuhudiwa hivi karibuni katika mji wa Johannesburg ambapo walioathirika zaidi ni wale wanaoishi katika vijiji na vitongoji duni, mvua za Durban zimewaathiri wote wanaoishi katika maeneo ya watu masikini na vilevile ya matajiri.

Maoni