Apr 25, 2019 07:47 UTC
  • Wakuu wa Baraza la Mpito la Kijeshi la Sudan wajiuzulu

Viongozi watatu kati ya 10 wa Baraza la Mpito la Kijeshi la Sudan wametangaza kujiuzulu, huku wananchi wa nchi hiyo wakitazamiwa kuendelea na maandamano yao leo Alkhamisi, kulishinikiza jeshi likabidhi madaraka kwa raia.

Viongozi hao wa kijeshi waliojiuzulu jana Jumatano ni Maluteni Jenerali Omar Zain al-Abdin, Jalaluddin Al-Sheikh na Al-Tayieb Babikir. Viongozi hao serikali ya mpito ya Sudan wametangaza kujiuzulu muda mfupi baada ya kufanyika mkutano kati ya wawakilishi wa jeshi na viongozi wa waandamanaji uliofanyika jana Jumatano usiku.

Baada ya mkutano huo, jeshi lilitangaza kuwa limefikia makubaliano kwa mambo mengi miongoni mwa matakwa ya waandamanaji. Pande hizo mbili ziliafikiana kuunda kamati ya pamoja ili kutatua tofauti zao.

Awadh Ibn Auf, kamanda wa jeshi aliyechukua uongozi wa nchi baada ya kung'lewa Bashir, na akajiuzulu siku chache baadaye

Duru za habari zinaarifu kuwa, viongozi hao wakuu wa Baraza la Mpito la Kijeshi la Sudan wamejiuzulu baada ya kutuhumiwa kuwa walikuwa na ushirikiano wa karibu na utawala uliopinduliwa.

Itakumbukwa kuwa, Rais Omar al-Bashir alipinduliwa mnamo Aprili 11 baada ya maandamano ya miezi kadhaa ya wananchi; na hivi sasa  Baraza la Kijeshi la Mpito chini ya uongozi wa  Luteni Jenerali Abdel Fattah al Burhan Abdelrahman limechukua madaraka kwa muda. 

Tags

Maoni