• LRA iliwateka watu 296 kwenye robo ya kwanza ya 2016

Kundi la waasi la Lord's Resistance Army la Uganda liliwateka watu 296 katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika robo ya kwanza ya mwaka huu.

Ripoti iliyotolewa na shirika moja lisilo la kiserikali linalofuatilia waasi hao imeonya kuwa vitendo vya ghasia vya kundi hilo vinaongezeka.

Ripoti hiyo pia imesema wengi wa mateka hao ni kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati ambako watu 252 wametekwa wakiwemo watoto 57.

Kati ya watu wote 296 waliotekwa nyara, 200 walitoroka au kuachiliwa huru ndani ya siku chache. Baadhi ya mateka hutumiwa na waasi hao kubeba bidhaa zilizoporwa.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa kundi la waasi wa Uganda la Lord's Resistance Army (LRA) limeua zaidi ya watu laki moja na kuteka nyara watoto elfu sitini ambao baadhi yao wanatumiwa kama watumwa wa ngono.

Hivi sasa kikosi cha askari 3,000 wa Afrika kinachoongozwa na Uganda kinamsaka kiongozi wa LRA Joseph Kony, kikijumuisha pia askari wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Uganda, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kundi la waasi wa Kikristo la LRA liliasisiwa kaskazini mwa Uganda kwa shabaha ya kuasisi utawala nchini humo uliosimama juu ya amri kumi za Biblia. Taratibu waasi hao walipanua wigo wa harakati zao na kuvuka mpaka ambapo waliingia mashariki mwa Kongo na baadaye katika ardhi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Tags

Apr 25, 2016 04:04 UTC
Maoni