Jun 01, 2016 07:38 UTC
  • Mahakama ya Kodivaa yaanza kusikiliza kesi dhidi ya mke wa Gbagbo

Mahakama moja nchini Kodivaa imeanza kusikiliza kesi ya jinai za kivita inayomkabili Simone Gbagbo, mke wa Rais wa zamani wa nchi hiyo, Laurent Gbagbo.

Simone, ambaye alipandishwa kizimbani jana katika mahakama moja mjini Abidjan, alikanusha mashitaka dhidi yake, ambapo anadaiwa kuhusika na vita vya wenyewe kwa wenyewe, vilivyoripuka baada ya uchaguzi tata wa 2010, ambapo watu zaidi ya 3,000 waliuawa. Kesi hiyo ya jinai za kivita ni ya kwanza kufanyika katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika, ikizingatiwa kuwa serikali ilikataa kumkabidhi kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC. Licha ya Kodivaa kufungua kesi hiyo, lakini mashirika ya kutetea haki za binadamu likiwemo Shirikisho la Kimataifa la Haki za Binadamu linalowakilisha wahanga 250 wa machafuko hayo, yamejiondoa kwenye kesi hiyo yakisisitiza kuwa upande wa mashitaka haukufanya uchunguzi wa kina ili kuipa nguvu kesi hiyo.

Ni vyema kuashiria hapa kuwa, Januari 28 mwaka huu, Mahakama ya ICC iliyoko mjiniThe Hague nchini Uholanzi ilianza kusikiliza kesi dhidi ya rais wa zamani wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo, anayekabiliwa na tuhuma za kuhusika kwenye vurugu za baada ya uchaguzi mkuu nchini Kodivaa mwaka 2011. Mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo ya ICC, Fatou Bensouda anatafuta ushahidi wa kuthibitisha kuwa machafuko ya mwaka 2011 yalikuwa ya kuratibiwa na kwamba hatua ya Gbagbo ya kukataa matokeo ya uchaguzi baada ya kushindwa na mpinzani wake Allasane Ouattara ilikuwa sehemu ya mkakati huo wa kuzusha fujo.

Tags

Maoni