• ICC yamhukumu Bemba wa DRC miaka 18 jela

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imemhukumu miaka 18 jela Makamu wa Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jean-Pierre Bemba ambaye alikuwa anakabiliwa na tuhuma za kutenda jinai za kivita katika nchi jirani ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kati ya mwaka 2002-2003.

Akisoma hukumu hiyo hii leo kwa niaba ya jopo la majaji wa mahakama hiyo iliyoko mjini Hague nchini Uholanzi, Jaji Sylvia Steiner amesema ICC imemhukumu Bemba kifungo cha miaka 18 jela, kwa kupatikana na hatia ya kutenda jinai za kivita na dhidi ya binadamu kwa kuwatuma wapiganaji wa MLC katika Jamhuri ya Afrika ya Kati mwaka 2003 ili kusaidia kuzima mapinduzi ya kijeshi dhidi ya rais wa wakati huo, Ange -Felix Patasse.

Mashitaka dhidi ya Bemba yanajumuisha mauaji na ubakaji. Bemba ambaye aliwania urais dhidi ya Rais Joseph Kabila mwaka 2006, mwaka uliofuata alikimbia nchi na kueleka bara Ulaya kutokana kile alichokitaja kuwa 'kuhamishwa kwa lazima' na baadaye kukamatwa mwaka 2008.

Hukumu dhidi ya Bemba ni ya kwanza dhidi ya Makamu wa Rais wa zamani katika mahakama hiyo ya kimataifa iliyobuniwa mwaka 2002 mjini Hague nchini Uholanzi, ili kukabiliana na makosa ya jinai na haswa ya kivita. Mbali na hakumu ya leo, makamu huyo wa rais wa zamani wa Kongo DR anakabiliwa na kesi ya pili huko huko ICC pamoja na wapambe wake wanne wa karibu kwa tuhuma za kuwapa rushwa mashahidi wakuu katika kesi ya kwanza dhidi yake.

Tags

Jun 21, 2016 15:02 UTC
Maoni