• Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran alaani kimya kuhusu jinai za Saudia nchini Yemen

Khatibu wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran amelaani kimya cha jamii ya kimataifa kuhusu kuendelea jinai za utawala wa Saudi Arabia nchini Yemen na katika eneo la Mashariki ya Kati.

Hujjatul Islam wal Muslimin Kadhim Siddiqui Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya Tehran ameashiria jinai za Saudi Arabia nchini Yemen hasa mauaji ya raia wasio na hatia nchini humo waliokuwa katika ukumbi wa maombolezo hivi karibuni mjini Sana'a na kuongeza kuwa, kimya cha jamii ya kimataifa mbele ya jinai hizo za Saudia ni aibu kubwa na kashfa kwa wale wanaodai kutetea haki za binadamu akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Sheikh Siddiqui ameongeza kuwa, hatua ya Saudia kuwaua watoto nchini Yemen ni sawa na jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel ambao umekuwa ukiwaua watoto Wapalestina huko Ghaza na pia nchini Lebanon. Aidha amesema Saudi Arabia ni mshirika wa Marekani katika jinai zake Mashariki ya Kati.

Waumini katika Sala ya Ijumaa Tehran

Khatibu wa Sala ya Ijumaa pia ameashiria mazoezi ya Jeshi la Anga la Iran hivi karibuni na kusema, ujumbe wa luteka hiyo ni wa amani na urafiki kwa mataifa ya eneo na onyo kwa wale wote wanaolenga kuihujumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Sheikh Siddiqui pia ameashiria mkutano wa wiki hii wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na wasomi na watu wenye vipawa bora na maalum nchini Iran na kusema, vijana wenye vipawa katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wataibadilisha nchi hii kuwa yenye ustawi mkubwa na mbeba bendera kubwa ya ustaarabu wa Kiislamu.

Tags

Oct 21, 2016 13:45 UTC
Maoni