Nov 19, 2016 08:02 UTC
  • Hatua mpya ya Bunge la Marekani dhidi ya Iran

Wawakilishi wa Bunge la Marekani ambalo linadhibitiwa na Warepublican juzi walipasisha mpango ambao unazuia kuiuzia Iran ndege zaidi ya 100 za abiria aina ya Boeing.

Kwa kupasisha sheria hiyo, wabunge wa Marekani wanataka kuizuia serikali ya Obama kuharakisha kuiuzia Iran ndege hizo za abiria. Sheria hiyo mpya itaizuia Wizara ya Fedha ya Marekani kutoa kibali kwa taasisi za kifedha kwa ajili ya kutekeleza baadhi ya miamala inayohusiana na uuzaji au kuuzia upya Iran ndege za abiria. Sheria hiyo inapasa kupasishwa pia na Bunge la Seneti la Marekani. Serikali ya Barack Obama ambayo imebakiza wiki kadhaa sasa hadi kumaliza muda wake, ilishasema mara kadhaa kwamba Rais wa Marekani ataipigia kura ya veto sheria kama hiyo.

Hatua hiyo ya wabunge wa Marekani inapasa kutathminiwa kuwa ni sehemu ya harakati zilizo dhidi ya Iran na dhidi ya binadamu za Congresi ya Marekani. Hasa ikizingatiwa kwamba, ndege za abiria za Iran ni za zamani na kuna ulazima  wa kununuliwa ndege mpya ili kulinda maisha ya wasafiri. Wakati huo huo Iran inahitajia kuzikarabati na kununua ngege mpya za abiria ili kustawisha sekta yake ya utalii baada ya miaka kadhaa ya vikwazo.

Inaonekana kuwa, hatua hiyo ya wabunge wa Marekani imechukuliwa katika harakati mpya za Rais Mteule wa nchi hiyo, Donald Trump ambaye ameahidi kutazama upya makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 linalojumuisha Marekani (JCPOA) na vilevile kushadidisha vikwazo dhidi ya Iran. Jumanne iliyopita pia Bunge la Marekani lilichukua hatua nyingine dhidi ya Iran kwa kupiga kura 419 za ndio wakiunga mkono mpango wa kurefusha vikwazo vya miaka kumi dhidi ya Iran; sheria ambayo ilibuniwa mwaka 1996 kwa minajili ya kuyaadhibu makampuni ambayo yanawekeza katika sekta ya nishati ya Iran. Wabunge wa Marekani wamesema kuwa, wanataka  sheria ya vikwazo dhidi ya Iran iendelee kutekelezwa ili itoe ujumbe mzito kwamba, iwapo Tehran itakiuka vipengee vya makubaliano ya nyuklia, basi Marekani itatoao jibu kwa hatua hiyo na kwamba Rais yoyote wa Marekani anaweza kuvirejesha haraka vikwazo hivyo dhidi ya Iran.

Rais Mteule wa Marekani Donald Trump

Ukweli ni kuwa kwa kuzingatia ushindi waliopata Warepublican katika uchaguzi wa rais wa Novemba 8 ambao umewafanya wadhibiti Congresi ya nchi hiyo na idadi nyingine ya magavana katika majimbo mbalimbali ya Marekani, ilitarajiwa kuwa Warepublican hao wangeanza kufanya  jiitihada kubwa za kuwasilisha mipango ambayo ingepelekea kuzidishwa vikwazo dhidi ya Iran na au kufuta na kusimamisha hatua zilizochukuliwa katika uwanja huo na serikali ya Obama kuhusiana na makubaliano ya JCPOA. Mwenendo huo wa Wamarekani dhidi ya Iran umepingwa na nchi za Ulaya waitifaki wa serikali ya Washington. Bi Federica Mogherini ambaye ni Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya anaona kuwa, makubaliano ya JCPOA si makubaliano ya pande mbili tu za Iran na Marekani bali ni makubaliano yaliyofikiwa kati ya Iran na nchi za kundi la 5+1 ambayo Marekani ni miongoni mwa nchi hizo na kwamba azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepasisha kisheria makubaliano hayo na kutoa dhamana ya utekelezaji wake.

Federica Mogherini Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya

Wakati huo huo nchi nyingine wanachama wa kundi la 5+1 yaani Russia na Uchina pia zinapinga harakati hiyo ya Warepublican wa Marekani dhidi ya Iran. Msimamo usio wa kimantiki wa Congresi ya Marekani kuhusu makubaliano ya JCPOA na vilevile kupinga kwake suala la kuondolewa Iran vikwazo linapaswa kupewa mazingatio makubwa hasa katika upande kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetekeleza kikamilifu vipengee vya makubaliano hayo  kama walivyokiri washirika wa Ulaya wa Washington, na kwa msingi huo Marekani haina kisingizio chochote cha kutoyatekeleza makubaliano hayo.

Tags

Maoni