Mar 21, 2017 02:47 UTC
  • Ujumbe wa Nairuzi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi; sisitizo juu ya utambulisho na izza ya taifa la Iran

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ametoa ujumbe maalumu kwa mnasaba wa kuanza mwaka mpya wa 1396 hijria shamsia.

Katika ujumbe wake huo, Ayatullah Khamenei ametoa mkono wa heri na baraka kwa mnasaba wa maadhimisho ya kuzaliwa Bibi Fatimatuz-Zahra (sa) na kwa mnasaba wa Sikukuu ya Nairuzi kwa Wairani wote, hususan familia adhimu za mashahidi na waliojitolea mhanga vitani, ambapo mbali na kuuombea mwaka 96 uwe mwaka wa baraka, amani na hali bora ya maisha kwa wananchi wa Iran na Waislamu wote duniani, aliupa mwaka huu mpya jina la mwaka wa ”Uchumi wa Muqawama: Uzalishaji na Ajira”.

Kwa muda wa karibu miongo minne tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, taifa la Iran limevikiuka vigingi vya changamoto na vitisho vingi. Sehemu kubwa ya changamoto hizo ni matatizo yaliyotokana na siasa za Marekani na madola ya Magharibi zenye nia ya kulidhuru taifa la Iran. Hivi sasa pia sio tu vitisho hivyo havijakwisha bali vinaendelea kuratibiwa upya kwa kutumia mbinu za kuvuruga uchumi wa Iran. Kwa zaidi ya miongo mitatu sasa Marekani imeiwekea Iran anuai za vikwazo; lakini matokeo ya vikwazo hivyo yamekuwa ni kuzidi kuwa thabiti na imara zaidi taifa la Iran. Ujumbe wa mwaka mpya wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi umetilia mkazo tena nukta hiyo muhimu. Kama alivyoashiria Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi, mwenendo wa harakati hiyo ya jitihada kubwa na isiyosita umeinua izza ya Iran na kuufanya upate nguvu zaidi utambulisho wa taifa la Iran kulikoshuhudiwa katika matukio yote ya mwaka 95 kiasi kwamba maadui wa kila pembe ya dunia walikiri kuhusu nguvu, uwezo na adhama liliyonayo taifa la Iran.

Wairani wakiwa katika haram ya Imam Ridha (as) wakati wa kuingia mwaka mpya wa 1396 hijria shamsia

Taifa la Iran linauanza mwaka mpya katika hali ambayo mbali na jitihada hizo zilizoandamana na mafanikio limekuwa na hali ya kuridhisha pia katika uga wa uthabiti na usalama. Kwani licha ya majirani zake pamoja na nchi kadhaa za eneo kukumbwa na vita, machafuko na mvurugiko wa amani, Iran imeupita mwaka 1395 hijria shamsia ulioshuhudia dhoruba nyingi za ukosefu wa amani kieneo na kimataifa, ikiwa na “amani thabiti na endelevu”.

Mafanikio iliyopata Iran ambayo yameshuhudiwa katika mazingira ya amani na uthabiti licha ya kukabiliwa na vizuizi na mashinikizo yameonyesha kuwa harakati ya kusonga mbele taifa hili haiwezi kukwamishwa wala kusitishwa. Na hivi ni vipimo vya ustawi na maendeleo. Kwa sababu hiyo, kutokana na uelewa kamili alionao juu ya vita vya kiuchumi vya adui na malengo yake ya kushadidisha mashinikizo na vikwazo dhidi ya Iran, Kiongozi Muadhamu amekuwa akitilia mkazo kila mara umuhimu wa kuimarisha miundomsingi ya uchumi na udharura wa kuzingatia suala hilo kupitia kaulimbiu ya “Hatua na Vitendo”. Kuhusiana na nukta hiyo, Ayatullah Khamenei amebainisha mikakati ya kati na ya muda mrefu kupitia kaulimbiu za kiuchumi alizotoa katika jumbe za kuanza mwaka mpya ikiwa ni pamoja na “Urekebishaji Mtindo wa Matumizi”, “Kufanya Hima ya Ziada na Kazi ya Ziada”, “Mwaka wa Jihadi ya Uchumi” na “Uchumi na Utamaduni- Azma ya Kitaifa na Uongozi wa Kijihadi”, kaulimbiu ambazo zimetoa mwanga wa kujenga uchumi imara wa muqawama unaoandamana na ustawi. Ni kwa msingi huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi aliupa mwaka uliopita wa 1395 jina la mwaka wa “Uchumi wa Muqawama; Hatua na Vitendo” na akatilia mkazo tena suala hilo muhimu kwa kuupa mwaka huu wa 96 jina la mwaka wa “Uchumi wa Muqawama: Uzalishaji na Ajira”.

Mwaka mpya wa Kiirani huanza sambamba na msimu wa machipuo

Hakuna shaka yoyote kuwa mojawapo ya njia za kufikia kwenye usalama endelevu wa kiuchumi ni kuendeleza njia ya uchumi wa muqawama. Kwa hakika ujumbe wa mwaka mpya wa Ayatullah Khamenei umetoa taswira ya wazi ya kuelewa maana ya usalama wa kiuchumi, ambapo mbali na kubainisha umuhimu na udharura wa kuzingatia suala hilo na kupongeza hatua zilizochukuliwa hadi sasa amesisitiza kuwa jitihada za kutoa athari zenye kuhisika zaidi zinapasa ziendelezwe katika nyuga zote.

Hakuna shaka yoyote kuwa ulegevu na ugoigoi wowote utakaofanywa katika uimarishaji uchumi utalifanya taifa liwe rahisi kuathirika na mashinikizo ya adui ambayo kila mwaka yanazidi kuongezeka na kwa mbinu tata zaidi. Kama alivyoashiria Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi katika ujumbe wake wa Nairuzi, mahudhurio makubwa na ya hamasa ya wananchi katika maandamano ya Bahman 22 ya maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu lilikuwa jibu kwa dharau iliyoonyeshwa na Rais wa Marekani kama ambavyo kujitokeza kwa wingi wananchi hao katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds kulidhihirisha utambulisho na malengo matukufu yanayofuatiliwa na wananchi wa Iran; na utambulisho na malengo hayo matukufu ni sisitizo la azma waliyonayo wananchi hao ya kuyafikia malengo makubwa katika mustakabali.../

 

Tags

Maoni