• Ayatullah Siddiqi: Hujuma ya Marekani huko Syria, ni kinyume cha sheria za kimataifa

Khatibu wa Sala ya Ijumaa katika mji wa Tehran amesema kuwa, shambulizi la Marekani nchini Syria siku ya Ijumaa iliyopita, linakinzana na sheria zote za kimataifa.

Ayatollah Kadhim Siddiqi  ameyasema hayo katika hotuba ya Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo hapa mjini Tehran ambapo sambamba na kuashiria hujuma hiyo ya kijuba ya Marekani dhidi ya Syria na kwa madai yasiyo na msingi wowote ya utumiwaji wa silaha za kemikali na serikali ya Damascus, amesema kuwa hatua ya upande mmoja, ya kikatili na iliyofanyika bila kibali, ni kinyume na sheria zote za kimataifa.

Maandalizi ya Iran ya Kiislamu kwa ajili ya kumkabili adui yeyote

Khatibu wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran amezitaka nchi zote za dunia kuzuia mwenendo huo wa kichokozi unaofanywa na Marekani dhidi ya nchi nyingine. Kadhalika amesisitiza kuwa taifa na jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limejiweka tayari kukabiliana na chokochoko zozote tarajiwa za adui na kwamba kwa kutegemea nguvu ya imani, uwezo wa kitaifa na nyenzo zake yenyewe, Iran itatoa jibu kali litakalomfanya adui ajute. Khatibu wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran sambamba na kukosoa vikali kimya cha jamii ya kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa kuhusiana na mwendelezo wa uvamizi na jinai kubwa za Saudia na waungaji mkono wake huko nchini Yemen, amesema kuwa ni suala lisilo na shaka yoyote kwamba, Aal Saud na marafiki wao ikiwemo Marekani, Israel na mataifa mengine, watapata jibu kali kwa jinai za mauaji ya raia wasio na hatia na waliodhulumiwa wa Yemen na kadhalika siasa zao za kuibadili Yemen kuwa ardhi iliyochomeka.

Uchaguzi nchini Iran

Katika sehemu nyingine, Khatibu wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran amesisitizia ushiriki mkubwa wa wananchi katika uchaguzi ujao wa rais na mabaraza ya miji hapa nchini na kueleza kwamba suala hilo litaimarisha uwezo wa kitaifa na ni jibu kwa maadui wa Iran. Amesema kuwa, ushiriki mkubwa katika masanduku ya kupigia kura kuna maana ya kujadidisha kiapo na baia wananchi wa Iran kwa malengo matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.

Tags

Apr 14, 2017 15:05 UTC
Maoni