• Larijani: Inafedhehesha nchi za Kiislamu kuafikiana na utawala wa Kizayuni na Marekani kuwaua Waislamu

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) ya Iran amesema ni jambo la kufedhehesha kwa baadhi ya nchi za Kiislamu kuafikiana na utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani juu ya kuwavurumizia mabomu ya vishada Waislamu.

Ali Jarijani aliyasema hayo jana alipohutubia ufunguzi wa mashindano ya 34  ya kimataifa ya Qur'ani Tukufu yanayofanyika hapa mjini Tehran. Alisema machungu makubwa zaidi uliyonayo leo Ulimwengu wa Kiislamu ni ya hitilafu kati ya nchi za Kiislamu na kuongeza kuwa harakati za kigaidi na ukufurishaji zinawadunisha Waislamu.

Dakta Larijani amebainisha kuwa kitendo cha makundi ya kigaidi cha kuzitumbukiza kwenye mgogoro nchi za Kiislamu kimeyafungulia njia ya kujiingizia kwenye nchi hizo madola ya nje ya eneo hili.

Mashindano ya kimataifa ya Qur'ani ya mjini Tehran

Huku akiashiria kwamba makundi hayo ya kigaidi na ukufurishaji yameupatia fursa ya kupumua utawala wa Kizayuni, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema baadhi ya nchi za Kiislamu zinahatarisha maisha ya Waislamu wa eneo hili kwa kuusaidia nyuma ya pazia utawala wa Kizayuni huku zikiuchukulia kuwa ni wa kirafiki uhamasishaji zinaopewa na Marekani na utawala wa Kizayuni.

Spika wa Bunge aidha amekosoa kuutumia ugaidi kimaslahi kunakofanywa na madola ya Magharibi na kubainisha kuwa Magharibi inautumia vibaya uungaji mkono wa baadhi ya nchi za Kiarabu kwa hatua za makundi ya kigaidi.

Dakta Larijani amesisitiza kuwa hakuna hoja ya kuhalalisha hitilafu, migogoro na mapigano kati ya nchi za Kiislamu.

Mashindano ya 34 ya kimataifa ya Qur'ani Tukufu yalifunguliwa rasmi jana hapa mjini Tehran yakihudhuriwa na washiriki 276 wa usomaji na kuhifadhi Qur'ani kutoka nchi 83..../

Apr 20, 2017 07:07 UTC
Maoni