• Hatua kwa hatua kuelekea kwenye uchaguzi wa rais wa Iran, majina ya wagombea yatangazwa

Baraza la Kulinda Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Alkhamisi ya jana lilitangaza majina ya watu sita waliotimiza masharti ya kugombea kiti cha Rais katika uchaguzi ujao na kuyatuma kwa Wizara ya Mambo ya Ndani.

Taarifa iliyotolewa na Tume ya Uchaguzi ya Iran imesema, watu sita waliokamilisha masharti ya kugombea kiti cha Rais hapa nchini ni Sayyid Mustafa Agha Mir Saliim, Is'haq Jahangiri Koshai, Hassan Rouhani, Sayyid Ebrahim Raeisi Sadati, Muhammad Baqir Qalibaf na Sayyid Mustafa Hashemi-taba.

Uchaguzi wa 12 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ule wa mabaraza ya miji na vijiji umepangwa kufanyika tarehe 19 Mei kote nchini. Uchaguzi huo unapewa mazingatio maalumu katika duru mbalimbali za kisiasa na vyombo vya habari. Hata hivyo jambo lililomulikwa zaidi katika kipindi hiki ni majina ya watu waliopasishwa kugombea kiti cha Rais wa Iran kati ya makumi ya wanasiasa mashuhuri waliokuwa wametangaza utayarifu wao kwa ajili ya kugombea nafasi hiyo. Wakati wa kuandikishwa majina ya wagombea urais, idadi kubwa ya wanasiasa mashuhuri na mamia ya watu wengine walijiandikisha kwa ajili ya kushiriki katika kinyang'anyiro hicho.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hakuna kizuizi chochote kinachowazuia raia kujiandikisha kwa ajili ya kugombea kiti cha Rais kwa masharti na vigezo maalumu. Kwa msingi huo ni jambo lililotarajiwa tangu hapo awali kujitokeza idadi kubwa ya wagombea wa kiti cha Rais. Hata hivyo Baraza la Kulinda Katiba linalazimika kuchunguza ustahiki wa wale wote wanaojiandikisha kwa ajili ya kugombea nafasi hiyo na kuona kama wametimiza masharti yaliyoainishwa na Katiba. Kwa mujibu wa Ibara (9) kifungu cha 115 cha Katiba, ustahiki wa waombea wote wa kiti cha Rais unapaswa kuchunguzwa na kupasishwa na Baraza la Kulinda Katiba kabla ya kufanyika zoezi hilo. Kifungu hicho kinasisitiza kuwa, mgombea kiti cha Rais anapaswa kuwa muirani asili na mwenye uraia wa Iran, awe na uwezo wa utendaji na ujuzi wa kutatua matatizo mbalimbali, awe na historia ya kuwa mtu mwema, mwaminifu, mchamungu na muumini, awe na imani kwa misingi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na dini rasmi ya nchi.

Tunapotazama orodha ya majina sita yaliyopasishwa na Baraza la Kulinda Katiba kwa ajili ya kugombea kiti cha Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tunaona sura ya mirengo mbalimbali ya kisiasa. Kila mmoja wao ni miongoni mwa shakhsia mashuhuri wa kisiasa na wamekuwa na tajiriba ya kiutendaji ya miaka mingi katika nafasi na maeneo tofauti.

Kwa sasa mbio za kuelekea kwenye uchaguzi wa Rais zinashika kasi zaidi na zaidi na hapana shaka kuwa, kila uchaguzi una nguzo mbili: Nguzo ya kwanza ni ushiriki wa wananchi ambao unahalalisha zoezi hilo na kuwa na taathira katika mustakbali wa kisiasa wa nchi, na nguzo ya pili ni wagombea wanaojiarifisha kubeba majukumu na dhima ya uongozi.

Sasa wagombea sita waliopasishwa kushiriki katika kinyang'anyiro hicho wamekabidhiwa medani ya kuanza kujinadi na kutangaza sera zao kwa wananchi. Katika kipindi hiki wagombea hao watatumia majukwaa mbalimbali kufanya kampeni na kutetea sera na siasa zao, suala ambalo kwa kawaida huwa kama injini inayowahamasisha wananchi kushiriki kwa wingi katika zoezi la uchaguzi. Hivyo basi kadiri kampeni za uchaguzi zinavyofanyika kwa njia bora zaidi, ndivyo hamu ya wananchi ya kutaka kushiriki katika zoezi hilo inavyozidi, suala ambalo ndilo msingi wa mfumo wa kidemokrasia.    

Apr 21, 2017 14:27 UTC
Maoni