• Zarif: Marekani imekiuka makubaliano ya nyuklia ya JCPOA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mara nyingine tena amesisitiza kwamba Marekani haijatekeleza majukumu yake mkabala na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Muhammad Javad Zarif leo Ijumaa ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa Marekani imekiuka roho na matini ya makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na nchi za kundi la 5+1 maarufu kama JCPOA. Zarif ameyasema hayo akijibu matamshi yaliyotolewa hivi karibuni ya Rais wa Marekani. 

Rais Donald Trump wa Marekani jana Alhamisi alidai katika kikao cha pamoja na waandishi wa habari akiwa pamoja na Paolo Jentiloni, Waziri Mkuu wa Italia katika ikulu ya  White House kuwa Iran haiheshimu roho na muhtawa wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Rais Trump akiwa White House na Waziri Mkuu wa Italia, Paolo Gentiloni 

Trump ametoa madai hayo katika hali ambayo ripoti mbalimbali za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zimekiri kuwa Iran  imekuwa ikitekeleza wajibu wake kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Vilevile Bi Federica Mogherini, Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya hivi karibuni alisisitiza kuwa makubaliano ya JCPOA ni ya jamii ya kimataifa na kwamba si makubaliano ambayo yanapangwa na pande mbili pekee na kuweza kubadilishwa na pande hizo.

Federica Mogherini, Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya  

Iran na kundi la 5+1 linazoundwa na nchi za Uingereza, Ufaransa, Russia, China, Marekani pamoja na Ujerumani tarehe 14 Julai mwaka juzi zilisaini makubaliano kuuhusu miradi ya nyuklia ya Iran; ambao yalianza kutekelezwa tarehe 16 mwezi Januari mwaka jana. 

Apr 21, 2017 15:43 UTC
Maoni