• Khatibu wa Swala ya Ijumaa Tehran: Mahudhurio makubwa ya wananchi katika uchaguzi yatadhihirisha nguvu ya Iran

Khatibu wa Swala ya Ijumaa katika mji wa Tehran amesema kuwa kushiriki kwa wingi wananchi wa Iran katika uchaguzi ujao, kutaonyesha nguvu na uwezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Akizungumza kwenye hotuba za Swala ya Ijumaa hapa Tehran, Ayatullah Muhammad Muvahhedi Kermani amesisitiza kuwa wananchi wanapasa kuzingatia umuhimu wa suala la uchaguzi na kueleza kuwa: Wananchi wa Iran kwa mahudhurio yao makubwa kwenye uchaguzi ujao, watadhihirisha namna Mfumo wa Kiislamu wa Iran unavyoungwa mkono na wananchi.

Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran ameashiria kwamba wananchi wanapasa kutilia maanani nukta chanya na hasi za wagombea na kubainisha kuwa: Wagombea walioidhinishwa wasitoe ahadi zisizotekelezeka. Ayatullah Muvahedi Kermani amesema kuwa kutomuogopa adui hususan Marekani ni miongoni mwa sifa anazopaswa kuwa nazo Rais wa Jamhuri ya Kiislamu.

Swala ya Ijumaa Tehran

Ayatullah Muvahhedi Kermani pia ameashiria mashambulizi ya hivi karibuni ya Marekani dhid ya kituo cha anga cha jeshi la Syria cha al Shayirat katika mkoa wa Homs na kueleza kuwa: Uvamizi wa Marekani huko Syria hauwezi kusahaulika.

Khatibu wa Swala ya Ijumaa katika mji wa Tehran ameashiria ukhabithi na jinai zinazofanywa kila uchao na Marekani na kubainisha kuwa, Marekani siku zote inajaribu kila iwezalo kuzidhoofisha nchi nyingine ili ziangamie. 

Tags

Apr 21, 2017 16:23 UTC
Maoni