• Waziri wa Ulinzi Iran: Kushiriki kwa wingi Iran katika uchaguzi

Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa Ijumaa ndio kinga kubwa zaidi ya kuyazuia madola ya kibeberu yanayotoa vitisho dhidi ya Iran.

Brigedia Jenerali Hussein Dehqan ameyasema hayo leo mjini Tehran alipozungumza na wafanyakazi wa Wizara ya Ulinzi. Dehqan ameashiria hali ya sasa katika eneo na kusema Marekani, Utawala wa Kizayuni na Utawala wa Saudia zinapanga njama ya kuendeleza mgogoro, vita na umwagaji damu  katika fremu ya NATO ya Kiarabu. Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema kwa kuonyesha mshikamano, umoja na uwezo wa kitaifa katika uhchaguzi, taifa la Iran litaweza kuvunja njama hizo zilizojaa shari.

Brigedia Jenerali Dehqan amesema kujitokeza kwa wingi wananchi katika upigaji kura Ijumaa kutadhamini uhai na kuendelea kudumu Mapinduzi ya Kiislamu sambamba na kustawi na kunawiri Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Wagombea watano wa kiti cha urais ni Mostafa Aqa-Mirsalim ambaye ni waziri wa zamani wa utamaduni na muongozo wa Kiislamu, Es'haq Jahangiri makamu wa kwanza wa serikali ya sasa, Ibrahim Raisi Sadat Msimamizi wa Haram ya Imam Ridha AS pamoja na rais wa sasa anayetetea nafasi yake Hassan Rouhani. Hapo jana Meya wa Tehran Mohammad Baqer Qalibaf alitangaza kujiondoa katika mchuano wa kuwania urais na kusema anamuunga mkono Ibrahim Raisi.

Wagombea kiti cha urais Iran

Uchaguzi wa 12 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unatarajiwa kufanyika Ijumaa ya tarehe 19 mwezi huu wa Mei sambamba na uchaguzi wa tano wa mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji kote nchini. 

Kamati ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema Wairani zaidi ya milioni 56 wametimiza masharti ya kupiga kura na hivyo wanatazamiwa kushiriki katika uchaguzi ujao wa urais.

Wairani wanaoishi nje ya nchi wataweza kupiga kura katika vituo 269 vya upigaji kura vilivyoko katika ofisi 131 za kidiplomasia za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nchi 103 kote duniani.

Tags

Mei 16, 2017 13:38 UTC
Maoni