• Waziri wa Usalama wa Taifa nchini Iran: Harakati zote za adui zinafuatiliwa kwa karibu

Waziri wa Usalama wa Taifa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, askari wa usalama wa nchi hii watatoa jibu kwa njama yoyote ya maadui.

Sayyid Mahmoud Alavi ameyasema hayo Ijumaa ya leo baada ya kushiriki katika upigaji kura wa uchaguzi wa rais wa duru ya 12 na uchaguzi wa duru ya tano wa mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji nchini hapa ambapo amewambia waandishi wa habari kwamba, uelewa wa maafisa usalama wa taifa hili na uwezo wao wa kiintelijensia ndio umeweza kutambua na kusambaratisha harakati zenye lengo la kuchafua usalama na amani katika kipindi cha uchaguzi. 

Seyyed Ebrahim Raisos-Sadati, mmoja wa wagombea wa urais

Sayyid Alavi ameongeza kuwa, hadi sasa hakuna harakati au mrengo wowote ulio dhidi ya mapinduzi ya Kiislamu au dhidi ya usalama ulioweza kutia dosari shughuli ya upigaji kura nchini hapa. Kadhalika Waziri wa Usalama wa Taifa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameelezea ushiriki wa wananchi katika uchaguzi kuwa unaodumisha usalama na amani ya Iran. Duru ya 12 ya uchaguzi wa rais na kadhalika duru ya tano ya uchaguzi wa mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji ulianza asubuhi ya Ijumaa ya leo nchini Iran.

Wairan waishio nje ya nchi wakishiriki upigaji kura

Katika uchaguzi wa huo, Seyyed Ebrahim Raisos-Sadati, Hassan Rouhani, Sayyid Mostafa Agha Mirsalim na Mostafa Hashemitaba wamechuana vikali. Kadhalika uchaguzi huo umefanyika katika zaidi ya nchi 100  duniani, ambapo Wairan wanaoishi nje ya nchi nao wameshiriki katika zoezi hilo.

Tags

Mei 19, 2017 16:23 UTC
Maoni