Mei 20, 2017 13:20 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Mshindi wa uchaguzi ni wananchi wa Iran na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ujumbe maalumu kwa mnasaba wa uchaguzi wa jana Ijumaa (Mei 19, 2017) wa Iran na kusema kuwa, mshindi wa uchaguzi huo ni wananchi wa Iran na mfumo Jamhuri ya Kiislamu ambapo licha ya kuweko njama nyingi za maadui, lakini uchaguzi huo umevutia umati mkubwa wa wananchi wa taifa hili kubwa kwa namna bora kabisa.

Ayatullah Khamenei amesema hayo na kuongeza kuwa, kushiriki kwa wingi mkubwa wananchi katika uchaguzi huo na kupanga foleni ndefu hadi kufikia kwenye masanduku ya kupigia kura katika kila kona ya Iran na kushirikisha wananchi wa matabaka yote kunaonesha wazi namna demokrasia ya Kiislamu ilivyokita mizizi humu nchini.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema, kwa mara nyingine Iran ya Kiislamu imewashinda nguvu wenye chuki na uadui na taifa hili na kubainisha kwamba, baada ya uchaguzi huo wananchi wanapaswa kurejea katika umoja na mshikamano wao kwani bila ya shaka yoyote hiyo ni moja ya mambo yanayoimarisha nguvu za taifa, Amesema, kila mmoja anapaswa kutoa mchango wake katika jambo hilo ili aweze kusaidia katika jukumu la kuiletea maendeleo nchi na kuiongoza upande wa kufanikisha malengo yake makuu. 

Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

 

Ayatullah Khamenei aidha amemtaka Rais mteule na wote watakaokuwemo kwenye serikali yake wafanye kazi kwa bidii kubwa na kiungwana ili kuiondolea nchi matatizo yake, kamwe wasighafilike na washikamane vilivyo na njia hiyo iliyonyoka, wawazingatie watu wa tabaka la chini, walipe kipaumbele suala la kuimarisha maisha ya vijijini na maeneo ya watu maskini na wapambane vilivyo na ufisadi pamoja na matatizo yote ya kijamii.

Vile vile amewashukuru wote waliofanikisha uchaguzi huo uliofanyika katika mazingira ya haki, utulivu na amani  kama ambavyo pia amelishukuru shirika la Sauti na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB) kwa mchango wake mkubwa katika suala hilo.

Rais Hassan Rouhani ametetea kiti chake cha urais katika uchaguzi uliofanyika jana Ijumaa Mei 19, 2017, kwa kupata zaidi ya kura milioni 23.

Uchaguzi nchini Iran

 

Tags

Maoni