• Iran yalaani utawala wa Kizayuni kwa kuufunga Msikiti wa Al Aqsa

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kuufunga Msikiti wa Al Aqsa na kuzuia sala ya Ijumaa msikitini hapo na kuonya kuwa, hatua hizo zitakuwa na matokeo hatari sana.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Bahram Qassemi Jumamosi alisema hatua hiyo ya Israel inaenda kinyume na misingi ya haki za binadamu na sheria za kibinadamu.

Aidha amesema utawala wa Kizayuni mbali na jinai  na vitendo vyote vya kuhujumu haki za kimsingi za Palestina sasa utawala huo umelenga uhuru na haki ya kuabudu ya Waislamu wa Palestina.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza ulazima wa kufunguliwa tena Msikiti wa al Aqsa haraka iwezekanavyo huku akitoa wito kwa nchi zote huru duniani na taasisi za kimataifa kuushinikiza utawala dhalimu wa Israel uzingatie haki za Wapalestina.

Bahram Qassemi

Itakumbukwa kuwa Ijumaa asubuhi Wapalestina waliwapiga risasi na kuwaangamiza wanajeshi wawili wa utawala wa Kizayuni wa Israel na baada ya hapo askari wa Kizayuni waliokuwa hapo waliwapiga risasi na kuwaua shahidi vijana watatu Wapalestina.

Kufuatia tukio, hilo utawala wa Kizayuni wa Israel uliufunga msikiti wa Al Aqsa na kuwazuia Waislamu kusali sala ya Ijumaa na hadi sasa msikiti huo umefungwa. Aidha Wazayuni walimkamata kwa muda Imamu wa Msikiti wa Al Aqsa Sheikh Muhammad Hussein aliyesalisha Ijumaa barabarani nje ya msikiti huo. Hii ni mara ya kwanza kwa sala ya Ijumaa kutosaliwa katika Msikiti wa Al Aqsa tokea mwaka 1969.

Jul 16, 2017 06:39 UTC
Maoni