• Jasusi mwingine wa Marekani atiwa mbaroni nchini Iran

Msemaji wa Chombo cha Mahakama cha Iran amesema kuwa, jasusi mmoja mwenye uraia wa nchi mbili ukiwemo wa Marekani ambaye aliingia nchini Iran kwa ajili ya kufanya ujasusi, ametiwa mbaroni na wizara ya usalama wa taifa ya Iran.

Shirika la habari la IRIB limemnukuu Gholam Hossein Mohseni Ejei, msemaji wa Chombo cha Mahakama cha Iran akisema leo mbele ya waandishi wa habari hapa mjini Tehran kwamba, jasusi mmoja Mmarekani ambaye ana pia uraia wa nchi nyingine (si Iran) ametiwa mbaroni na wizara ya usalama wa taifa humu nchini na baada ya kusailiwa imethibitika kwamba alikuwa amekusanya taarifa za kijasusi kwa ajili ya kuipatia Marekani kuhusiana na Iran.

Jasusi Mzayuni

 

Mohseni Ejei ameongeza kuwa, baada ya kutiwa mbaroni, jasusi huyu amekabidhiwa kwa chombo cha mahakama na tayari hivi sasa ameshahukumiwa kwenda jela miaka 10.

Vile vile amesema, jasusi huyo ana haki ya kukata rufaa, na iwapo atafanya hivyo, atawekewa wakili wa kumtetea mahakamani ili uadilifu uweze kutendeka.

Shirika la Kijasusi la Marekani CIA

Hii si mara ya kwanza kwa Marekani kutuma majasusi wake nchini Iran. Mara kwa mara wizara ya usalama wa taifa ya Iran imekuwa ikiwatia mbaroni majasusi wa Marekani katika maeneo mbalimbali humu nchini hususan ya mipakani.

Jul 16, 2017 15:19 UTC
Maoni