Mkuu wa Idara ya Mahakama nchini Iran amesema kuwa, ushindi wa vikosi vya wananchi na jeshi la Iraq katika kuukomboa mji wa Mosul, umesambaratisha heshima ya Marekani na madola mengine ya kibeberu.

Ayatullah Sadeq Amoli Larijani ameashiria kukombolewa mji wa Mosul wa Iraq kutoka mikomoni mwa magaidi wa Daesh na kubainisha kwamba, ushindi wa kambi ya muqawama huko Mosul umeipelekea Marekani ifanye mashambulio ya mabomu dhidi ya kambi ya muqawama huko Syria.

Mkuu wa Idara ya Mahakama nchini Iran ameashiria nafasi muhimu ya uongozi wa Marjaa, vikosi vya kujitolea vya wananchi na himaya ya kiushauri ya Iran katika operesheni ya kuukomboa mji wa Mosul kutoka kwa magadi wa Daesh na kubainisha kwamba, magaidi hao walikuwa wakitaka kupandikiza donda lingine la saratani katika Mashariki ya Kati kama lile la utawala wa Kizayuni wa Israel, lakini Alhamdulilahi wameshindwa kufikia lengo lao hilo chafu.

Vifaru vya jeshi la Iraq katika operesheni dhidi ya magaidi wa Daesh

Itakumbukwa kuwa, Haider Jawad Kadhim Al-Abadi Waziri Mkuu wa Iraq tarehe kumi mwezi huu alitangaza kukombolewa kikamilifu mji wa Mosul kutoka mikononi mwa magaidi wa kitakfiri wa Daesh, ushindi ambao unatathminiwa kuwa pigo kubwa kwa magaidi hao na waungaji mkono wake.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, serikali ya nchi hiyo hivi sasa inafanya juhudi za kurejesha uthabiti na kukabiliana na changamoto zinazoikabili baada ya kutoa pigo kwa wanamgambo magaidi na wakufurishaji wa Daesh. 

Jul 17, 2017 14:11 UTC
Maoni