• Majibu ya Iran kwa Kongresi ya Marekani, Washington inavuruga usalama M. ya Kati

Kamati ya Usalama wa Taifa na Siasa za Nje ya Bunge la Iran imepasisha mpango kamili wa kukabiliana na chokochoko na ugaidi wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati.

Mpango huo wa kukabiliana na sera za uhasama na kigaidi za Marekani una vipengee kadhaa ikiwa ni pamoja na kuainisha stratijia za kukabiliana na vikwazo vya Marekani, jinsi Marekani inavyounga mkono ugaidi, ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na serikali ya Washington, adhabu na hatua za kulipiza kisasi na jinsi ya kuwalinda raia wa Jamhuri ya Kiislamu. Mpango huo ambao utapigiwa kura katika kikao cha wazi cha Bunge la Iran Jumapili ijayo umetayarishwa kwa ajili ya kukabiliana na sheria iliyopasishwa na Kongresi ya Marekani kwa anwani eti ya "Sheria ya Kukabiliana na Hatua Haribifu za Iran 2017".

Congesi ya Marekani

Serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani inafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba, inadhoofisha makubaliano ya nyuklia ya Iran na kundi la 5+1 na kuiarifisha Tehran kuwa inavuruga na kutishia usalama wa eneo la kistratijia la maghaibi mwa Asia. Serikali ya Trump pia, kinyume na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kwa kisingizio cha kukabiliana na eti hatua haribifu za Iran, inafanya njama za kudhoofisha uwezo wa kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu, kuituhumu Iran kuwa inaunga mkono ugaidi na kukiuka haki za binadamu na hiyo kuhalalisha utekelezaji wa sheria ya vikwazo dhidi ya Iran.

Ni katika mazingira hayo ndipo Bunge la Iran likabuni mpango kamili wa kukabiliana na sheria ya Kongresi ya Marekani kwa shabaha ya kuainisha vipengee vya uharibifu unaofanywa na nchi hiyo katika eneo la magharibi kwa Asia ikiwa ni pamoja na harakati zake za kuunga mkono ugaidi, mauaji ya watu wasio na hatia na ukiukaji wa haki za binadamu ndani na nje ya Marekani.

Makombora ya Iran yanaitia kiwewe Marekani 

Moja kati ya masuala muhimu yaliyomo katika mpango kamili wa Bunge la Iran wa kukabiliana na vikwazo vya Marekani, ni kutangaza uungaji mkono wake kwa kazi za Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah) za kuimarisha uwezo wa kijeshi wa Iran. Kwa kutumia kisingizio cha uwezo wa makombora ya Iran na majaribio ya makombora hayo, Marekani imetoa tafsiri yake binafsi na kutaja majaribio hayo kuwa yanakiuka azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Madai hayo ya Marekani yanalenga kuinyima Iran usalama wa kuaminika na kutegemewa na hatimaye kulilenga shabaha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah) ambalo limekuwa na mchango muhimu sana katika kuimarisha uwezo wa kiulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu. Katika uwanja huo Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Bahram Qassemi anasema: “Madai hayo hayana ukweli wala msingi, kwa sababu uwezo wa makombora ya Iran ni suala la ndani na la kujilinda na halina mfungamano wowote na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama”. 

Bahram Qassemi

Miongoni mwa mambo yaliyopewa kipaumbele na kuzingatiwa katika mpango kamili wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu wa kukabiliana na chokochoko na ugaidi wa Marekani ni kuhusu tathmini ya uungaji mkono na misaada ya fedha na silaha ya serikali ya Washington kwa makundi ya kikatili na kigaidi ya Mashariki ya Kati kama Daesh na Jabhatu Nusra. Sera za kindumakuwili za Marekani kuhusiana na ugaidi zimeyasababishia hasara kubwa na zisizoweza kufidika mataifa ya eneo la Mashariki ya Kati ikiwemo Iran. Kwa msingi huo mchambuzi wa masuala ya siasa wa Marekani, Mike Harris, alisema tarehe 8 Agosti katika mahojiano yake ya televisheni ya Press kwamba, Marekani imefanya jinai za kivita katika eneo la Mashariki ya Kati na kusisitiza kuwa: "Jeshi la Marekani linawaunga mkono magaidi wa ISIS (Daesh) huko Iraq na Syria", mwisho wa kunukuu.

Aug 12, 2017 02:18 UTC
Maoni