• Bunge lapitisha hoja ya mpango wa kukabiliana na harakati za kigaidi za US Mashariki ya Kati

Wabunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) wameunga mkono na kupitisha hoja ya mpango wa kukabiliana na harakati za chokochoko na za kigaidi za Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati.

Akisoma ripoti ya Kamati ya Usalama wa Taifa na Sera za Nje ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu bungeni leo kuhusu mpango wa kukabiliana na Marekani, msemaji wa kamati hiyo Sayyid Hossein Naqavi Hosseini, amesema mpango wa kukabiliana na hatua za chokochoko na za kigaidi za Marekani katika eneo umechunga misingi ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) wa makubaliano ya nyuklia na kwamba mapendekezo yaliyowasilishwa kutekelezwa katika mpango huo hayakinzani na JCPOA.

Sayyid Hossein Naqavi Hosseini

Naye Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na mkuu wa timu ya Iran katika kamati ya kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa JCPOA amesisitiza kwamba mpango uliopendekezwa na Bunge ni sehemu ya hatua zilizopitishwa na kamati hiyo ya usimamizi wa makubaliano ya nyuklia kwa ajili ya kukabiliana na mpango uliopendekezwa na Kongresi ya Marekani dhidi ya Iran. 

Araqchi ameongeza kuwa Wizara ya Mambo ya Nje inakubaliana nao na kuunga mkono mpango ulioafikiwa na Bunge kwa ajili ya kukabiliana na Marekani.

Abbas Araqchi

Mpango huo wa kukabiliana na harakati za chokochoko na kigaidi za Marekani katika Mashariki ya Kati una sehemu tisa zinzojumuisha nukta kuu, maana za maudhui, kuainisha stratijia za kukabiliana na vikwazo vya Marekani, uungaji mkono wa Marekani kwa ugaidi, ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na serikali ya Washington, adhabu na hatua za kulipiza kisasi, namna ya kukabiliana na vikwazo vya kiuchumi vya Marekani na jinsi ya kuwalinda raia wa Jamhuri ya Kiislamu.

Mnamo Juni 15 mwaka huu Seneti ya Marekani iliendeleza hatua za nchi hiyo za kiadui na kihasama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu kwa kupitisha mpango kamili wa vikwazo dhidi ya Iran uliopewa jina la eti "Sheria ya Kukabiliana na Hatua Haribifu za Iran 2017".../

Aug 13, 2017 08:11 UTC
Maoni