Rais Donald Trump wa Marekani hivi karibuni alidai kuwa Iran haiheshimu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Akijibu matamshi hayo ya Trump, Muhammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: Ili kuepuka kutengwa kwa kisingizio cha kutaka kujiondoa katika makubaliano ya JCPOA, Donald Trump anafanya kila linalowezekana kuidhihirisha Iran kuwa ndiyo iliyokiuka makubaliano hayo . 

Zarif amesema kuwa, madai ya Trump yanaonyesha nia mbaya ya Marekani sambamba na kukiuka makubaliano ya nyuklia ya kundi la 5+1.

Makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na nchi wanachama wa kundi la 5+1 maarufu kwa kifupi kama (JCPOA) ni mwafaka uliopasishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi Julai mwaka 2015 baada ya kusainiwa na nchi husika katika mazungumzo ya nyuklia. 

Abbas Araqchi Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran juzi Ijumaa alisisitiza katika hotuba aliyoitoa kwenye Taasisi ya Amani ya Sasakawa nchini Japan kuhusu makubaliano ya JCPOA na tathira zake katika ngazi ya kimataifa na kieneo kwamba: Makubaliano hayo yana nafasi kuu katika uga wa kimataifa na  kwamba yanaungwa mkono na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na jamii nzima ya kimataifa.   

Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran  

Araqchi amesema kuwa visingizio vya Marekani na hatua yake ya kuiwekea Iran vikwazo kwa sababu ya miradi yake wa makombora ni jambo lilisokubalika na kwamba miradi ya makombora ya Iran ni matunda ya uwezo wa wananchi. Ameongeza kuwa: Miradi hiyo ni kwa ajili ya kujilinda.

Hata hivyo Rais Trump wa Marekani anasisitiza suala la kujiondoa katika makubaliano hayo kwa kutumia visingizo visivyo vya nyuklia. Jarida la Marekani la Dallas News limekosoa hatua zinazochukuliwa na kiongozi wa nchi hiyo kuhusu makubaliano ya nyuklia na Iran zikizitaja kuwa ni za kustaajabisha na kuandika kuwa: Donald Trump mwezi Oktoba mwaka huu ataingaza Iran kuwa imekiuka makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015, uamuzi ambao utaipatia Marekani uwezo wa kumuadhibu vikali kiuchumi mtu yoyote anayefanya biashara na Tehran. Gazeti hilo limesema kuwa: Hatua hiyo haina taathira yoyote na hakuna nchi yoyote iliyoshiriki katika mazugumzo ya nyuklia ya mwaka 2015 inayounga mkono misimamo hiyo ya Trump. 

Rais Donald Trump wa Marekani 

Pamoja na hayo yote Marekani kwa mara kadhaa sasa imeonyesha namna isivyotambua mpaka wowote katika kukiuka makubaliano ya kimataifa na mfano wa karibuni kabisa wa jambo hilo ni kujiondoa nchi hiyo katika mkataba wa mabadiliko ya tabia nchi. Hata hivyo katika kadhia ya JCPOA Marekani inakabiliana na changamoto kubwa hususan katika uwanja wa biashara ya kimataifa. Huwenda Marekani ikaweza kuzuia biashara moja kwa moja kati ya Iran, mashirika na taasisi za kifedha na kiuchumi za nchi hiyo lakini ni suala lisilokubalika kutekeleza marufuku hiyo kwa nchi nyingine ikiwemo China au Umoja wa Ulaya. Kwa msingi huo Trump anatafuta njia ya kutaka kuidhihirisha Iran kuwa imekiuka makubaliano ya JCPOA na kwamba ndiyo iliyochukua hatua ya kwanza ya kukiuka makubaliano hayo.  

Aug 13, 2017 08:19 UTC
Maoni