• Rais Rouhani: Makubaliano ya JCPOA ni kwa maslahi ya Iran, Mashariki ya Kati na ulimwengu

Rais Hassan Rouhani amesema kuwa, makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) ni kwa maslahi ya Iran, Mashariki ya Kati na ulimwengu kwa ujumla na kwamba, kila atayetaka kuyadhuru makubaliano haya atakuwa amejidhuru yeye na nchi yake.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hayo leo katika kikao cha Baraza la Mawaziri ambapo ameashiria matamshi ya hivi karibuni yaliyo dhidi ya makubaliano ya JCPOA ya Rais Donald Trump na kubainisha kwamba, madai ya Rais wa Marekani kwamba, JCPOA ndio makubaliano mabaya kabisa katika historia ya Marekani hayana ukweli kwani kile ambacho kimo katika makubaliano hayo ni kufaidika pande zote mbili na si faida kwa upande mmoja na hasara kwa upande wa pili.

Wawakilishi katika mazungumzo ya nyuklia ya Iran na kundi la 5+1

Rais Hassan Rouhani amesema bayana kwamba, kama Marekani  itataka kuchukua hatua dhidi ya makubaliano hayo ya nyuklia ya JCPOA, ulimwengu mzima utasimama dhidi yake, kwani  mataifa ya ulimwengu yako dhidi ya mtu yeyote atayetaka kuyadhoofisha makubaliano haya ya kimataifa.

Aidha Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria ushiriki wa viongozi 130 wa kigeni, wawakilishi wa nchi 105 na jumuiya za kimataifa katika sherehe ya kuapishwa kwake baada ya uchaguzi wa 12 wa Rais wa Iran iliyofanyika Jumamosi iliyopita hapa mjini Tehran na kusisitiza kwamba, baadhi ya watu wanataka kuonyesha kwamba, Iran imetengwa, lakini ulimwengu umepaza sauti na kutangaza kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijatengwa.

Aug 13, 2017 13:33 UTC
Maoni