• Ukosoaji wa Kiongozi Muadhamu kwa kimya cha jumuiya za kimataifa na kutochukua hatua kuhusiana na maafa ya Myanmar

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekosoa vikali kimya na kutochukua hatua jumuiya za kimataifa na wanaojidai kuwa watetezi wa haki za binadamu kuhusiana na matukio ya maafa yanayojiri Myanmar na kusisitiza kwamba, njia ya ufumbuzi wa kadhia hiyo ni nchi za Kiislamu kuchukua hatua za kivitendo na kuishinikiza kisiasa na kiuchumi serikali isiyo na huruma ya Myanmar.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo asubuhi ya leo wakati wa kuanza darsa ya "masomo ya juu kabisa ya fikihi" ambapo sanjari na kusisitiza ulazima wa nchi za Kiislamu kuchukua hatua za kivitendo amesema kuwa, makusudio ya kuchukua hatua za kivitendo si kupeleka majeshi, bali nchi za Kiislamu zinapaswa kuzidisha mashinikizo ya kisiasa, kiuchumi na kibiashara dhidi ya serikali ya Myanmar na kupaza sauti zao dhidi ya jinai hizi katika jumuiya za kimataifa.

Kadhia ya Myanmar na dhulma inayohalalishwa dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya chimbuko lake ni njama zilizoratibiwa ambapo katika hilo kunaonekana mlolongo wa mauaji ya kizazi na dhulma ya kihistoria dhidi ya Waislamu. Umma wa Kiislamu umewahi kupitia mara moja dhulma hii katika kadhia ya Palestina na hujuma za kikatili za Wazayuni watenda jinai na magaidi.

Maandamano ya kulaani mauaji dhidi ya Waislamu wa Myanmar

Filihali, ulimwengu wa Kiislamu unashuhudia kukaririwa senario hiyo nchini Myanmar. Hii ni katika hali ambayo, mkono wa Wazayuni, Marekani na Waingereza uko wazi katika maafa haya ambayo hatupaswi kuyafumbuia macho na kama alivyosema Kiongozi Muadhamu ni kuwa, tusiwe ni wenye kutosheka tu na kuyataja au kuyaelezea katika kalibu ya mapigano ya kidini.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, si sahihi kuyahafifisha maafa ya Myanmar kwa kuyaeleza kuwa ni mapigano ya kidini tu baina ya Waislamu na Mabudha na akaongeza kwa kusema kuwa, Tabaan, yumkini katika kadhia hii taasubi za kidini nazo pia zikawa na taathira, lakini kadhia hii ni ya kisiasa. Hii ni kwa sababu mtendaji wake ni serikali ya Myanmar na katika nafasi ya juu kabisa ya serikali hiyo kuna mwanamke asiye na huruma ambaye ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel; na ukweli ni kwamba matukio yanayojiri ni sawa na kifo cha tuzo ya amani ya Nobel.

Aung San Suu Kyi, Mshauri Mkuu wa Serikali ya Myanmar na mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel

Inasikitisha kwamba, hali ya maisha ya jamii ya Waislamu Warohingya sio tu kwamba, haijaboreka tangu Aung San Suu Kyi ashike hatamu za uongozi bali imezidi kuwa mbaya. Huu ni ukweli ambao unafumbiwa macho na akthari ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa au umesahauliwa.

Kile ambacho kinatokea nchini Myanmar si suala la hatima na majaaliwa ya Waislamu milioni moja wa Myanmar, bali matukio haya ni mlolongo wa njama dhidi ya Uislamu na jamii ya Kiislamu kwa kuwapachika nembo ya ugaidi na misimamo ya kufurutu ada.

Vipi mtu anaweza kuuelezea ukandamizaji, mauaji na mateso wanayokabiliwa nayo Waislamu Warohingya wa Myanmar?

Waislamu Warohingya wa Myanmar wakiyahama makazi yao kukimbia hujuma dhidi yao katika jimbo la Rakhine

Wimbi jipya la ukandamizaji na mauaji ya jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu wa Rohingya katika jimbo la Rakhine la magharibi mwa nchi hiyo lilianza tarehe 25 Agosti mwaka huu.

Hadi sasa zaidi ya Waislamu elfu sita wa Kirohingya wameuawa huku wengine elfu nane wakijeruhiwa. Ukubwa wa jinai hizo unayafanya majukumu na masuuliya ya asasi za kimataifa kama Umoja wa Mataifa  na Baraza la Haki za Binadamu kuwa mazito zaidi.

Ni kwa kusisitizia nukta hiyo ndipo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamju sambamba na kukosoa hatua ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ya kutosheka tu na kutoa maneno ya kulaani jinai za Myanmar akabainisha kwamba, wanaojidai kuwa ni watetezi wa haki za binadamu ambao baadhi ya wakati huzusha makelele wakati inapotokea mhalifu mmoja akahukumiwa katika nchi fulani hawaonyeshi radiamali yoyote kuhusiana na mauaji na kufanywa wakimbizi makumi ya maelfu ya watu nchini Myanmar.

Ni kwa mintarafu hiyo ndio maana mzigo wa jukumu hili la kihistoria zaidi uko katika mabega ya nchi za Kiislamu; na Ulimwengu wa Kiislamu unapaswa kutoa ujumbe wa wazi na mzito kuhusiana na Myanmar.

 

Sep 12, 2017 11:30 UTC
Maoni