• Iran na Afrika Kusini kuimarisha uhusiano wao wa Kibunge

Hossein Amir-Abdollahian, Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya Kimataifa wa Bunge la Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu na Afrika Kusini zinaweza kutumia uwezo wao kuondoa vizuizi vilivyopo ili kuimarisha uhusiano wa pande mbili ukiwemo wa kibunge.

Abdollahian ameyasema hayo leo Jumanne hapa mjini Tehran baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Afrika Kusini nchini Iran, William Max Whitehead.

Ameongeza kuwa, uhusiano imara wa mabunge ya nchi mbili hizi unaweza kutumiwa kuimarisha zaidi ushirikiano wa Iran na Afrika Kusini katika nyuga za uchumi, siasa na utamaduni.

Kwa upande wake, Balozi wa Afrika Kusini mjini Tehran ambaye anamaliza muda wake amesisitiza kuwa, kuimarika uhusiano wa kibunge wa nchi mbili hizi kumekuwa na nafasi chanya katika kuboreka masuala ya mawasiliano wa Tehran na Pretoria hususan katika nyuga za uchumi na biashara.

Kadhalika amesisitizia haja ya kupanua ushirikiano katika sekta binafsi.

Baleka Mbete, Spika wa Bunge la Afrika Kusini aliyeitembelea Iran hivi karibuni

Mapema mwezi uliopita, wanadiplomasia wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Afrika Kusini walifanya mazungumzo hapa mjini Tehran kuhusu namna ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili hususan katika uga wa siasa.

Kuimarisha uhusiano na nchi za Afrika ni katika ajenda kuu ya sera za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Rais Hassan Rouhani wa Iran amekuwa akisisitiza kuwa, Tehran itaendelea kuimarisha uhusiano wake na nchi za Afrika katika nyuga za uchumi, siasa na utamaduni.

Sep 12, 2017 15:00 UTC
Maoni