• Rais Rouhani katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Augustine Mahiga.
    Rais Rouhani katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Augustine Mahiga.

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kustawisha uhusiano na nchi za Afrika ni katika misingi ya siasa za nje za Iran na amesisitiza kwamba, Tehran inakaribisha kwa mikono miwili suala la kuimarisha uhusiano na ushirikiano wake na nchi zote za Afrika ikiwemo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Rouhani amesema hayo katika mazungumzo yake hapa mjini Tehran na Augustine Mahiga Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuitaja Tanzania kama lango la Iran kuingia katika soko la Afrika Mashariki.

Rais Rouhani amesema kuwa, uhusiano wa kihistoria na kiutamaduni wa miaka 900 wa mataifa haya mawili, ni rasilimali yenye thamani kubwa katika njia ya kupanuliwa zaidi ushirikiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais wa Iran ameashiria kuweko tayari mashirika ya Iran yenye uwezo katika uga wa teknolojia na uhandisi kuendeleza miradi ya ustawi barani Afrika ikiwemo Tanzania na kuongeza kwamba, ushirikiano wa kiuchumi unapaswa kuwa kwa kiwango cha uhusiano wa kihistoria, kiutamaduni na kisiasa kati ya Iran na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Rais Rouhani kadhalika amesema kuwa, ugaidi ni tatizo kubwa kwa dunia nzima na kwamba, magaidi wako kila mahala wakiwa na majina tofauti, lakini lengo lao ni moja na bila ya shaka nchi zote zinapaswa kuungana katika vita vya kupambana na tatizo hizo.

Kwa upande wake Augustine Mahiga Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania amesema kuwa, nchi yake imeazimia kustawisha uhusiano wake na Iran katika nyanja zote na kueleza kwamba, Tanzania inayakaribisha nchini humo mashirika ya Iran kwa ajili ya kusukuma mbele mipango yake ya maendeleo.

Oct 11, 2017 16:50 UTC
Maoni