• Iran na Tanzania zasisitiza udharura wa kuimarisha uhusiano wa kiuchumi

Waziri wa Masuala ya Uchumi wa Iran na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania wamesisitiza udharura wa kuimarishwa uhusiano wa kiuchumi baina ya pande mbili.

Hayo yalisemwa Jumatano mjijni Tehran katika mkutano baina ya Waziri wa Masuala ya Uchumi Iran Masoud Karbasian na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Augustine Mahiga. Katika kikao hicho, Karbasian alisema kuongezeka kiwango cha uhusiano wa kibiashara kunategemea kutekelezwa mapatano yaliyofikiwa baina ya nchi mbili.

Karbasian ameashiria safari ya Mahiga nchini Iran na kusema moja ya malengo yake ni kuandaa safari tarajiwa ya Rais Hassan Rouhani wa Iran nchini Tanzania. Ameelezea matumaini kuwa kutashuhudiwa ongezeko la kiwango cha mabadilishano ya kibiashara baina ya nchi mbili.

Katika kikao hicho, Mahiga ameashiria uhusiano mzuri uliopo baina ya Iran na Tanzania na kusisitiza umuhimu wa hali hiyo kuendelea kuimarika.

Rais Hassan Rouhani wa Iran na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Augustine Mahiga

Akizungumza na waandishi habari baada ya mkutano huo, Mahiga ameashiria mkopo ambao Tanzania ilipokea kutoka Iran miaka ya nyuma na kusema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekubali kutopata faida katika mkopo huo na mazungumzo zaidi kuhusu mkopo huo yatafanika wiki ijayo."

Mahiga ameishukuru serikali na taifa la Iran kwa kuiunga mkono Tanzania na kuongeza kuwa, Iran imeipa Tanzania mikopo mingi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania aliwasili Tehran Jumatano akiongoza Ujumbe wa ngazi za juu ambapo ameshafanya mazungumzo na Rais Hassan Rouhani na mwenzake wa Iran Mohammad Javad Zarif.

Oct 12, 2017 05:36 UTC
Maoni