• Makubaliano ya nyuklia ya JCPOA; mtihani kwa Trump na itibari ya Marekani kimataifa

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA kwa kifupi, ni mtihani muhimu kwa serikali zilizoshiriki katika mazungumzo ya nyuklia na tawala nyingine duniani na kwamba, kutekeleza ahadi ni msingi wa dunia kuiamini serikali fulani.

Rais Hassan Rouhani alisema hayo Jumatano ya jana katika kikao na baraza lake la mawaziri, sanjari na kukaribia kutangazwa uamuzi wa mwisho wa serikali ya Trump kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kusisitiza kwamba, endapo pande zote za mazungumzo zitayaheshimu makubaliano hayo maana yake zitakuwa zimejilindia na kujihifadhia heshima zao na kama atatokea mtu na kutofungamana na makubaliano hayo, basi kwa hakika atakuwa amejiharibia mwenyewe heshima yake.

Wakati Iran na madola sita makubwa duniani yalipotiliana saini makubaliano ya nyuklia mwaka 2015 baada ya mazungumzo magumu ya miaka miwili, haikuwa ni kwa msingi wa kila mmoja kumuamini mwenzake. Kile ambacho kililetwa na makubaliano ya JCPOA ni kufikiwa makubaliano ambayo yaliungwa mkono na pande zote zilizoshiriki mazungumzo hayo na katika fremu ya ahadi za kimataifa ambapo hata azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliyaunga mkono makubaliano hayo na hivyo kuyapa sura ya kimataifa.

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Tangu siku ya kuanza ya kutekelezwa makubaliano hayo yaani Januari mwaka jana, kile ambacho kilikuwa kikidhamini utekelezwaji wa JCPOA hakikuwa ni makubaliano yaliyoko katika makaratasi, bali kuaminiana pamoja na nia njema ya pande za mazungumzo sambamba na kuwa na moyo wa kukubali majukumu ndilo lililokuwa sharti kuu la kuyafanya makubaliano hayo yatekelezwe.

Kwa kuzingatia kuwa, msingi wa itibari na kuaminiwa serikali fulani ni kuheshimu na kufungamana kwake na makubaliano ya kimataifa, mintarafu hiyo uzembe na upuuzaji wowote ule kwa msingi huu, kutaifanya nchi husika itangazwe mbele ya walimwengu kwamba, ni taifa lisilokubali kubeba majukumu au haliheshimu mikataba ya kimataifa. Hii leo baada ya kupita takribani miaka miwili ya utekelezwa wa JCPOA, makubaliano hayo yapo katika njia panda ya itibari na kutokuwa na itibari serikali ya Marekani.

Ishara zote za serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani zinaonyesha kuwa, makubaliano hayo yanaelekea upande wa kutoamianiana na jambo hilo kwa mara nyingine tena linawathibitikia wananchi wa Iran na walimwengu kwa ujumla kwamba, Marekani katu si nchi ya kuaminika.

Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya

Kuhusiana na jambo hilo, Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya alisema kuwa: Endapo Marekani itajitoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, itakuwa imezipatia ujumbe nchi nyingine za dunia kwamba, si nchi ya kuaminika na hiyo itatia alama ya swali itibari ya nchi hiyo kimataifa.

Aidha Bernie Sanders Seneta wa Marekani naye jana aliunga tena mkono makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kusisitiza kwamba: Kutoungwa mkono makubaliano hayo na Trump hakutakuwa na natija nyingine bighairi ya kutengwa Marekani

Kwa hakika bila kujali uamuzi utakaochukuliwa na serikali ya Trump kwa mujibu wa sheria za ndani za Marekani kuhusiana na kufungamana au kutofungamana Iran na JCPOA, au hatima itakayoyakumba makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji, ukweli wa mambo ni kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imejiandaa kwa machaguo yoyote yale.

Wajumbe wa mazungumzo ya nyuklia

Viongozi wa Iran wametangaza kinagaubaga kwamba, taifa hili halitafanya tena mazungumzo kuhusu JCPOA na lina mipango na mikakakati ya kukabiliana na uamuzi wowote ule wa serikali ya Trump.

Rais Rouhani amesisitiza kuwa: Hakuna wakati ambao wananchi wa Iran walikuwa na imani na Marekani na wanatambua kwamba, Washington ilichukua na inaendelea kuchukua hatua za namna gani dhidi ya maslahi ya taifa lao, lakini hii leo hayo yamewadhihirikia zaidi na hivi sasa wananchi hawa wameshikamana zaidi na bila shaka mkwamo tarajiwa wa makubaliano ya JCPOA hautakuwa na madhara yoyote katika njia ya kusukuma mbele gurumu la malengo na maslahi ya taifa hili la Kiislamu.

 

Tags

Oct 12, 2017 13:46 UTC
Maoni