• Sababu ya Wamarekani kuwa na hasira na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH

Waziri wa Ulinzi wa Iran ametoa radiamali yake kwa vitisho vya hivi karibuni vya serikali na viongozi wa Marekani dhidi ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusema kuwa, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni asasi kubwa kabisa iliyo dhidi ya ugaidi na iko mstari wa mbele katika vita na mapambano dhidi ya ugaidi katika Mashariki ya Kati.

Brigedia Jenerali Amir Hatami, alisema hayo Alkhamisi ya jana na kubainisha kwamba, Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH, jeshi na vikosi vingine vya Iran viko pamoja na vimesimama kidete kwa ajili ya kukabiliana na siasa na hatua za chuki, adawa na uzushaji mivutano na migogoro za serikali ya Marekani na kwamba, katu havitaruhusu usalama wa eneo hili uhatarishwe kupitia ugaidi na vita vya niaba.

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH ni moja ya nguzo muhimu na athirifu katika Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ambapo kulinda matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu na kukabiliana na njama za maadui wa mapinduzi haya ndio kazi muhimu kabisa ya asasi hii ya wananchi. Jeshi hili lilianzishwa  kwa tadbiri na ubunifu wa Imam Ruhullah Khomeini MA mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa lengo la kulinda misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu ambapo tangu wakati huo hadi sasa ikiwa tuko katika muongo wa nne wa mapinduzi haya, jeshi la SEPAH limekuwa na nafasi muhimu na kuwa dira ya kusonga mbele Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kupata nguvu kila leo katika nyuga mbalimbali hususan katika uwanja wa kijeshi.

Brigedia Jenerali Amir Hatami, Waziri wa Ulinzi wa Iran 

Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, maadui waliratibu na kuandaa mipango ya muda mfupi, kati na kati na muda mrefu kwa ajili ya kutoa pigo kwa mapinduzi haya.

Njama za kuyasambaratisha Mapinduzi ya Kiislamu zilikuwa katika orodha ya mipango na mikakati ya muda mrefu ya maadui. Hata hivyo njama hizo hazijaweza kufua dafu kutokana na kuweko nguvu muhimu kama Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na bila shaka hata katika mustakabali pia njama hizo hazitafanikiwa. Hili ndilo jambo lililoikasirisha na kuitia hasira Marekani.

Mbali na nafasi athirifu ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika nguvu na uwezo wa kisiasa wa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, kieneo pia SEPAH imeweza kuvifahamu vyema vitisho vinavyoikabili Iran na kisha ikavisambaratishia mbali. Kwa hakika ghaya na lengo kuu la kuanzisha vita vya niaba nchini Syria lilikuwa ni kukabiliana na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; lakini kuweko kwa nguvu zote jeshi la Sepah katika medani ya vita na magaidi wa kukodiwa wanaoungwa mkono na Marekani na Wazayuni kumesambaratisha kabisa malengo ya Marekani na washirika wake. Kutokuwa na ubavu Marekani wa kukabiliana moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kumewafanya Wamarekani wawe kila mara wakibuni njia za kuzitia doa na kuzichafulia majina nguzo mbalimbali za mfumo huu wenye nguvu.

Wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh 

Udiriki wa mambo wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran SEPAH sambamba na nafasi muhimu na yenye kuainisha mambo katika vita dhidi ya magaidi huko Syria na Iraq ni mambo yanayoweza kutathminiwa katika uwanja huu.

Kulionyesha jeshi la SEPAH mbele ya macho ya watu wa Mashariki ya Kati kwamba ni tishio ni njama za pamoja za Marekani na Wazayuni wakiungwa mkono na baadhi ya tawala za Kiarabu zenye fikra mgando na hivyo kuituhumu taasisi hii kwamba, eti inaunga mkono ugaidi, asasi ambayo imo katika harakati za kung'oa mizizi ya ugaidi katika eneo hili. Serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani inafanya juhudi za kuliweka jeshi la SEPAH katika orodha nyeusi ya nchi hiyo, katika hali ambayo, utendaji wa wanajeshi wa Marekani huko Syria na Iraq hauna tofauti yoyote na kundi la kigaidi la Daesh.

Rais Donald Trump wa Marekani

Kushambulia Marekani kwa makusudi maeneo ya raia huko Syria na Iraq, kuhama wakati wa usiku kutoka mahala pamoja hadi kwingine viongozi wa Daesh kwa kusaidiwa na Washington huko Syria sambamba na kuwafikishia silaha magaidi hao ni mifano ya wazi ya ya utendaji ulio sawa wa wanajeshi wa Marekani na kundi la kigaidi la Daesh.

Ukweli huu unaonyesha kuwa, harakati za serikali ya Rais Trump dhidi ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ikiwa nguzo muhimu yenye nguvu na inayopendwa zaidi dhidi ya ugaidi katika Mashariki ya Kati zina misingi ya chuki na uadui. Katika mazingira kama haya, hatua yoyote ile itakayochukuliwa na Marekani dhidi ya jeshi la SEPAH itakabiliwa na radiamali kali ya Iran. Kuhusiana na jambo hilo, Brigedia Jenerali Amir Hatami, Waziri wa Ulinzi wa Iran amesisitiza kwamba, hatua ya serikali ya Marekani ya kuliwekea vikwazo na kuliita jeshi la SEPAH kwamba ni la kigaidi yenyewe kwa hakika ni kitendo cha kigaidi.

Tags

Oct 13, 2017 08:13 UTC
Maoni