• Wanajeshi wa Marekani walipotiwa nguvuni na Jeshi la Sepah baada ya kuingia katika maji ya Iran kinyume cha sheria
    Wanajeshi wa Marekani walipotiwa nguvuni na Jeshi la Sepah baada ya kuingia katika maji ya Iran kinyume cha sheria

Kamati na Uhusiano wa Kimataifa ya Baraza la Congress la Marekani imepasisha azimio dhidi ya miradi ya makombora ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa ni kuonesha chuki zake za wazi dhidi ya Tehran.

Azimio hilo ambalo limewasilishwa mbele ya baraza hilo na Ed Royce, mkuu wa kamati ya uhusiano wa kimataifa ya Congress ya Marekani limeliwekea vikwazo Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH kwa madai ya eti kuendesha miradi isiyo halali ya kuimarisha makombora ya balestiki. Azimio hilo lililopewa jina la "Sheria ya Makombora ya Balestiki ya Serikali ya Iran na Uwekaji Vikwazo Kimataifa" limeifungulia njia serikali ya Marekani kuiwekea vikwazo vipya Iran.

Nembo ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH

 

Hatua hiyo ya kamati ya uhusiano wa kimataifa ya Congress ya Marekani imechukuliwa siku moja kabla ya serikali ya rais wa Marekani, Donald Trump kutangaza msimamo wake kuhusiana na namna ya kukabiliana na Iran pamoja na makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kwa jina maarufu la JCPOA. Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Congress la Marekani wanajaribu kuwa na msimamo mkali sawa na wa Donald Trump dhidi ya Iran na wanafanya njama za kila namna za kuhakikisha misimamo iliyo dhidi ya Iran inapata nguvu nchini Marekani. Sasa baada ya kuona kuwa dunia nzima imekiri kwamba Iran haina nia kabisa ya kumiliki silaha za nyuklia na imetekeleza kikamilifu makubaliano ya JCPOA, maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Marekani wameamua kuulenga kikamilifu muundo wa ulinzi wa Iran. Katika starijia za kiulinzi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, miradi ya makombora na kuimarisha miradi hiyo kunafanyika kwa lengo la kiulinzi tu kwa ajili ya kuiweka salama Iran katika eneo hili lenye migogoro mingi la magharibi mwa Asia.

Amma nukta ya kuzingatia hapa ni kwamba, katika makubaliano ya nyuklia baina ya Iran na kundi la 5+1 (JCPOA), hakuna hata mahala pamoja palipogusiwa miradi ya makombora ya Iran. Hata azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo limeunga mkono na kutia nguvu makubaliano ya JCPOA limeiomba tu Iran isitengeneze makombora yanayokusudia kubeba vichwa vya nyuklia. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kuwa utekelezaji wa azimio hilo la Umoja wa Mataifa ni wajibu wa kisheria. Ndio maana katika uimarishaji wa makombora yake, Iran inazingatia ustadi wa kulenga shabaha makombora yake na si kubeba vichwa vya nyuklia. Kwa maneno mengine ni kuwa, lengo la Iran si kuyafanya makombora yake yabebe vichwa vya nyuklia hivyo Tehran haijishughulishi na upande huo, bali inazingatia uwezo mkubwa wa makombora hayo ya kulenga shabaha kwa ustadi wa hali ya juu.

Wanajeshi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH ambao wamekuwa ni mwiba kwa Marekani na utawala wa Kizayuni baada ya kusambaratisha njama zao dhidi ya Iran na eneo la Mashariki ya Kati

 

Katika upande mwingine, Iran iko katika eneo ambalo baaadhi ya nchi zinatumia mamia ya mabilioni ya dola kujilimbikizia silaha na zinaweka mikataba mikubwa mikubwa ya silaha na Marekani na nchi za Ulaya, hivyo ni jambo la kawaida kabisa kwa Iran nayo kuwekeza katika uwezo wake wa makombora. Si hayo tu, lakini kwa makumi ya miaka sasa Iran imewekewa vikwazo vya silaha huku nchi za Magharibi zikizishehenesha baadhi ya nchi za eneo hili marundo ya silaha za kila namna. Sasa ni kichekesho kikubwa kuona nchi kama Marekani inaisakama Iran kwa kujiimarisha kiulinzi wakati yenyewe Marekani kila leo inawekeana na baadhi ya nchi za eneo hili la magharibi mwa Asia, mikataba ya silaha ya mabilioni ya dola. Bila ya shaka yoyote ni haki ya Iran ya kujiimarisha kiulinzi na kuhakikisha kwamba adui hafikirii kabisa kuivamia kijeshi.

Hii ni kusisitiza kuwa hatua ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH ya kushambulia ngome za magaidi wa Daesh nchini Syria kwa kutumia makombora yake ya masafa ya kati tena kutokea nchini Iran imewathibitishia walimwengu kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina mchezo katika suala zima la kulinda usalama wake. Tumalizie kwa kusema kuwa, vikwazo vya aina yoyote ile dhidi ya miradi ya makombora ya Iran ni kinyume cha sheria, si mantiki, lakini muhimu zaidi kuliko yote ni kwamba haviwezi kamwe kuizuia Iran kujiimarisha kiulinzi na kujidhaminia usalama wake.     

Oct 13, 2017 13:55 UTC
Maoni