• Brigedia Jenerali Ashtari: Matamshi ya Trump dhidi ya SEPAH yanadhihirisha upunguani wake

Mkuu wa Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, matamshi ya chuki na kiuadui ya Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH yanatokana na upunguani wake na kutofahamu kwake dunia.

Brigedia Jenerali  Hussein Ashtari amesema hayo katika hafla ya ufunguzi wa maonyesho ya kimataifa ya vifaa na zana za jeshi la polisi hapa mjini Tehran na kubainisha kwamba, mabeberu hususan Marekani wanapaswa kutambua kwamba, kuna mfungamano na mshikamano katika vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Mkuu wa Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kubainisha kwamba, hii leo Iran ipo katika eneo ambao linakabiliwa na machafuko, ameongeza kwamba  washauri wa kiusalama wa Iran wameweza kutoa msaada kwa nchi za eneo hili na hivyo kurejesha amani na usalama ambapo Iraq na Syria ni mfano wa wazi wa jambo hilo.

Rais Donald Trump  wa Marekani

Mkuu wa Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria matamshi ya Rais Donald Trum wa Marekani dhidi ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH na kubainisha kwamba, matamshi ya Trump yanathibitisha kwamba, kiongozi huyo wa Marekani ni punguani na hana ufahamu wowote kuhusu ulimwengu.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, stratijia ya Rais wa Marekani kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na misimamo yake ambayo imetajwa kuwa si ya kidiplomasia, imepingwa pia na viongozi wa nchi za Ulaya huku walimwengu wakitaka kuheshimiwa makubaliano hayo ya kimataifa yaliyofikiwa kati ya Iran na kundi la 5+1 linaloundwa na Ufaransa, Marekani, Uingereza, Russia, China pamoja na Ujerumani.

Tags

Oct 16, 2017 14:18 UTC
Maoni