• Kiongozi Muadhamu: Kuhitimishwa satwa ya Daesh ni pigo kwa Marekani na tawala tegemezi kwa Washington

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, kuhitimishwa satwa ya mti khabithi wa kundi la kigaidi la Daesh ni pigo kwa serikali za huko nyuma na za sasa za Marekani pamoja na tawala vibaraka na tegemezi kwa Washington katika Mashariki ya Kati ambazo zililianzisha kundi hili na kuliunga mkono kwa hali na mali ili zitanue satwa zao katika eneo hili na hivyo kuufanya utawala ghasibu wa Israel uwe na udhibiti wa eneo hili.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei  amesema hayo katika jibu lake kwa barua ya Meja Jenerali Qassem Suleimani Kamanda wa Kikosi cha Quds katika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kueleza kama ninavyonukuu: Ninamshukuru Mwenyezi Mungu Mkubwa ambaye amezipa baraka juhudi zako za kujitolea kijihadi pamoja na wenzako katika nyuga mbalimbali na hivyo kupelekea kung'olewa kwa mikono yenu nyinyi waja wema huko Syria na Iraq mizizi ya mti khabithi wa Daesh ambao mche wake ulipandwa na mataghuti wa dunia.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, hili sio pigo kwa kundi ovu na dhalimu la Daesh pekee, bali hatua hiyo ya kung'olewa mizizi ya Daesh imetoa pigo kubwa pia kwa siasa za kikhabithi za kuanzisha vita vya ndani katika Mashariki ya Kati na kuutokomeza muqawama ulio dhidi ya Israel sambamba na kuyadhoofisha madola na tawala huru kupitia viongozi waovu wa kundi hilo lililopotoka.

Meja Jenerali Qassem Suleimani Kamanda wa Kikosi cha Quds katika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Katika sehemu nyingine ya jibu lake kwa barua hiyo, Ayatullah Khamenei amemhutubu  Meja Jenerali Qassem Suleimani kwa kumwambia: Kwa hatua yako na wenzako ya kulisambaratisha donda hili angamizi la saratani, mumezihudumia pakubwa si nchi za Mashariki ya Kati na Ulimwengu wa Kiislamu pekee, bali mataifa yote na jamii nzima ya mwanadamu.

Kadhalika Ayatullah Khamenei ametoa mkono wa kheri na pongezi kwa ushindi huo na kubainisha kwamba, haipasi kughafilika na hila  na ghiliba za adui.

Tags

Nov 22, 2017 08:07 UTC
Maoni