• Mikusanyiko ya malalamiko nchini Iran na uungaji mkono wa Marekani; kukariri makosa yaliyopita

Kwa siku kadhaa sasa baadhi ya miji ya Iran imeshuhudia mikusanyiko na maandamano ya kulalamikia matatizo ya kiuchumi, kutojulikana hatima ya watu waliopata hasara na kupoteza fedha zao katika taasisi za fedha, ughali wa baadhi ya bidhaa na udhaifu wa serikali katika usimamizi.

Hata hivyo katika hatua iliyoratibiwa, baadhi ya mikusanyiko hiyo, imegeuka kuwa ya fujo na machafuko huku watu wenye nia ovu wakiitumia fursa ya maandamano hayo kushambulia majengo ya idara za serikali, benki na maeneo ya umma.

Akihutubia hapo jana  katika kikao cha kwanza cha duru ya tano ya baraza kuu la mikoa kilichofanyika mjini Tehran, Waziri wa Mambo ya Ndani Abdolreza Rahmani Fazli, alitoa jibu na radiamali kwa wale wanaotumia vibaya fursa ya mikusanyiko hiyo kufanya fujo na uharibifu nchini kwa kusisitiza kuwa, kamwe serikali haitoruhusu machafuko na uvunjifu wa amani.

Maandamano hayo yanayoungwa mkono na Marekani, Israel na Saudia

Alisema, uungaji mkono wa utawala wa Kizayuni na nchi zenye fikra mgando za eneo la Mashariki ya Kati pamoja na Marekani na kufurahishwa kwao na fujo na machafuko yaliyotokea nchini, kunadhihirisha ukweli halisi wa baadhi ya matukio yanayojiri hivi sasa nchini. Katika mwendelezo wa uungaji mkono huo Sarah Huckabee Sanders, Msemaji wa Ikulu ya Marekani (White House) asubuhi ya jana aliandika kwenye mtandao wa Twitter kwamba, Marekani iko pamoja na wafanya fujo na ghasia huku akitishia kwa kusema: "Siku za uvumilivu wa Marekani kwa ukandamizaji nchini Iran, zimefika kikomo."

Sarah Huckabee Sanders, Msemaji wa Ikulu ya Marekani

Nayo Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitoa taarifa yenye matamshi makali kwa kukariri kwa mara nyingine madai yaliyotolewa miezi kadhaa iliyopita na Rais wa nchi hiyo Donald Trump dhidi ya Iran kwa kudai kwamba mambo makuu yanayosafirishwa nje na Iran ni: "utumiaji nguvu, umwagaji damu na machafuko." Taarifa hiyo imebainisha pia kwamba, Washington inatoa mwito kwa "mataifa yote" kuwaunga mkono "waziwazi" watu wa Iran; ambao miezi michache tu iliyopita waliitwa na Trump kuwa ni magaidi.

Taifa la Iran limewahi kupata tajriba ya harakati za aina hiyo hapo kabla pia  na linaelewa vyema chimbuko na chanzo chake. Sura halisi ya njama na mipango iliyokusudiwa na Marekani ilidhihirika katika matamshi ya hivi karibuni yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Rex Tillerson.

Rex Tillerson, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani

Siku chache zilizopita gazeti la New York Times lilichapisha makala iliyoandikwa na Tillerson akisema: "Mapatano ya nyuklia ya Iran, hayana tena nafasi katika siasa zetu kuhusiana na Tehran....Hivi sasa sisi tuko katika hali ya kukabiliana na vitisho vyote vinavyosababishwa na Iran. Sehemu moja ya muelekeo huo inajumuisha uanzishaji tena wa muungano na washirika wetu katika eneo la Mashariki ya Kati....Na sisi tutachukua hatua kadhaa za kukabiliana na harakati za kuvuruga uthabiti katika eneo."

Hivi sasa Ikulu ya Marekani kupitia fremu ya ushirikiano wa kistratijia wa pamoja kati yake na Saudi Arabia na Israel wa kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina ndoto kuwa itaweza kuzigeuza vurugu hizo kuwa harakati kubwa ya machafuko ya ndani na mgogoro mkubwa katika eneo la Mashariki ya Kati.

Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ya mwaka 1979, Marekani ilichukua hatua kubwa kadhaa na kutosita kutekeleza kila njama kwa lengo la kuuangusha mfumo wa Kiislamu hapa nchini.

Rais Donald Trump wa Marekani

Katika uwanja huo hakuna njama yoyote chafu ambayo hadi sasa haijafanywa na Washington dhidi ya Iran ya Kiislamu kuanzia Vita vya Kulazimishwa vya miaka minane na kumuunga mkono kwa kila hali Saddam hadi kuiwekea Iran vikwazo, kuonyesha kuwa ni tishio mipango yake ya nyuklia, mbali na kujaribu kuchafua sura ya uwezo wa kiulinzi wa taifa hili. Hivi sasa pia Marekani inapanga njama nyengine mpya kwa lengo la kutoa pigo na kuidhuru Iran.

Viongozi wa serikali ya Trump wanaamini kwamba ili kuleta mabadiliko ya kweli katika mienendo ya Iran, ni lazima waubadilishe mfumo mzima wa utawala hapa nchini. Hapo kabla baadhi ya viongozi wa Marekani akiwemo Tillerson walitangaza mipango kadhaa ya kuleta mabadiliko ya kiutawala nchini lran, suala ambalo linadhihirisha malengo machafu yanayofuatiliwa na Marekani dhidi ya taifa hili.

Jumapili ya jana gazeti la New York Times liliashiria uungaji mkono ulioonyeshwa mara kadhaa na Trump kwa matukio yaliyotokea hivi karibuni nchini na kuandika kwamba: "Hadi sasa hakuna kinachoeleweka hasa juu ya malalamiko hayo au kwamba ni upi utakuwa mwisho wake." Lakini gazeti hilo limemhutubu Trump kwa kusema: "Hata kama Wairani watakuwa na fikra yoyote kuhusu serikali yao, lakini hawataki kuona rais wa Marekani, ambaye ni hivi karibuni tu alipinga kupatikana unafuu katika uchumi wa nchi yao sambamba kuwazuia kusafiri nchini Marekani, awe ndiye mtu wa kuwasemea kuhusu malalamiko yao."

Jan 01, 2018 11:26 UTC
Maoni