• Nchi mbalimbali zapinga uingiliaji wa Marekani katika mambo ya ndani ya Iran

Nchi kadhaa za eneo la Mashariki ya Kati zimetoa taarifa mbalimbali na kulaani uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Taarifa tofauti zimetolewa na nchi za Syria, Uturiki, Iraq, makundi ya Palestina na Lebanon na pia maafisa wa Russia kupinga uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya Iran.

Tokea Alhamisi wiki iliyopita, watu wa miji kadhaa ya Iran walijumuika na kutoa nara kulalamikia kutojulikana hatima ya waliofilisishwa na taasisi za kifedha, ughali wa baadhi ya bidhaa na udhaifu wa serikali katika usimamizi. Katika mijumuiko hiyo baadhi ya watu walitumia fursa hiyo vibaya na kuzusha fujo na ghasia.

Watawala wa Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel na vyombo vya habari ajinabi vimetumia vibaya mijumuiko hiyo na kupotosha mkondo wake na kuielekeza katika ghasia na fujo.

Waibua fujo wapatao himaya ya kigeni wameharibi mali za umma mjini Tehran na miji kadhaa ya Iran

Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imetoa taarifa ikilaani uingiliaji wa Marekani na utawala wa Kizayuni katika mambo ya ndani ya Iran. Pia Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki nayo imetoa taarifa kufuatia fujo za hivi karibuni nchini Iran na kusema utulivu na usalama wa Iran ni muhimu sana kwa Uturuki.

Nalo Baraza Kuu la Kiislamu la Iraq pia limesema njama za Marekani na Wazayuni dhidi ya Iran zitafeli. Naye mbunge wa ngazi za juu nchini Russia, Konstantin Kosachev ameonya kuwa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel zinashirikiana katika kuvuruga amani nchini Iran.

Harakati kadhaa za Lebanon ikiwemo Harakati ya Amal na Harakati ya Tauhidi ya Kiislamu zimetoa taarifa kulaani uingiliaji wa madola ya Magharibi na baadhi ya tawala za kieneo katika masuala ya ndani ya Iran.

Huko Palestina, Harakati ya Wananchi kwa Ajili ya Ukombozi wa Palestina nayo imetoa taarifa na kusema njama za Wazayuni na Wamarekani dhidi ya Iran zitafeli. 

Tags

Jan 03, 2018 04:02 UTC
Maoni