• Wairani waandamana kupinga fujo na machafuko na kuunga mkono Mfumo wa Kiislamu

Wananchi wa Iran kutoka pembe mbalimbali za nchi wamefanya maandamano hii leo kuuunga mkono Mfumo wa Kiislamu unaotawala sambamba na kulaani ghasia zinazoshuhudiwa katika baadhi ya maeneo.

Huku wakiwa wamebeba bendera za Iran, waandamanaji hao wamesikika wakipiga nara za kuiunga mkono serikali sanjari na kuwataka wenzao wanaozusha fujo katika baadhi ya maeneo kusitisha mwenendo huo.

Maandamano hayo ya kuunga mkono Mfumo wa Kiislamu yameshuhudiwa katika miji kama vile Ahvaz, Kermanshah, Bushehr, Abadan, Gorgan na Qom.

Wairani katika miji mingine wanatazamiwa kushiriki maandamano ya kuunga mkono Mfumo wa Kiislamu hapo kesho, huku wakazi wa mji mkuu Tehran, wakitazamiwa kuandamana kesho kutwa baada ya Swala ya Ijumaa.

Waandamanaji wanaouunga mkono Mfumo wa Kiislamu

Wiki iliyopita, maandamano ya amani ya Wairani waliokuwa wakilalamikia ughali wa maisha yalianza katika baadhi ya miji, lakini hatimaye yaligeuka na kuwa ya fujo huku baadhi ya waandamanaji, miongoni mwao wakiwa wamejizatiti kwa silaha wakifanya vitendo vya uhalifu kama kupora mali za umma na kuvamia vituo vya polisi na maeneo ya kidini.

Viongozi mbalimbali nchini wamelaani vitendo vya wanaofanya fujo katika maandamano hayo, huku Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akisema maadui wa Iran wametumia mbinu na njia mbalimbali walizonazo kama vile, pesa, silaha, siasa na muungano wa mashirika yao ya usalama ili kuibua matatizo katika Mfumo wa Kiislamu. 

Tags

Jan 03, 2018 15:38 UTC
Maoni